Unordered List


KAMATI KUU: MADIWANI BUKOBA HALALI



 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi  wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa kamati kuu wa kubatilisha kufukuzwa kwa madiwani wa Bukoba nje ya ukumbi wa NEC.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili na kutolea maamuzi pamoja na mambo mengine suala la Madiwani wanane waliotangazwa kufukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera.

Katika maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013 wa kuwafukuza uanachama Madiwani hao. Hivyo Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.

Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15). Ibara hiyo inasomeka kuwa moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo”.

Aidha, Kamati Kuu imewaonya Madiwani wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika Manispaa na Chama.

Kamati Kuu pia imeitaka Serikali kumwagiza mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali(CAG) kufanya ukaguzi maalum wa haraka wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na matokeo ya uchunguzi huo yasilishwe kwenye baraza la madiwani ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza Serikali za Mitaa.

Wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya zikichunguzwa; Kamati Kuu inawataka Madiwani wa CCM  kurejesha utulivu kwenye Manispaa na Chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.

Imetolewa na:-

Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM
ITIKADI NA UENEZI
27/08/2013

Chapisha Maoni

0 Maoni