Unordered List


Opportunity Education kutoa tablets kwa wanafunzi nchini

salma 74f14
Taasisi ya fursa ya Elimu (Opportunity Education) ya nchini Marekani imeazimia kuanzisha mradi wa laptop ndogo (tablets computer) kuanzia mwezi Januari mwaka 2014 nchini ambazo zitatumika kufundishia ili walimu waweze kufundisha haraka na kwa ufanisi zaidi pia wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza zaidi. (HM)

Hayo yamesemwa jana na Joe Ricketts ambaye ni mwanzilishi na mtendaji mkuu wa taasisi hiyo wakati wa hafla ya kuchangia uugwaji mkono wa utoaji elimu barani Afrika iliyoandaliwa na taasisi ya Malaika ya nchini humo na kufanyika katika chuo Kikuu cha Nebraska kilichopo mjini Lincoln .
Ricketts alisema mradi huo kwa mara ya kwanza utaanzia nchini Tanzania ambapo wanafunzi zaidi ya 1000 kutoka shule 10 tofauti watapewa laptop ndogo kwa ajili ya kusomea na baada ya kipindi cha mwaka mmoja watafanya mtihani ili kuangalia tofauti iliyopo kwa wale waliokuwa wakitumia na wasiotumia.
Baada ya majaribio hayo kama kutakuwa na mafanikio basi mradi huo utasambazwa katika shule nyingine nchini Tanzania ili kila mwanafunzi aweze kupata nafasi ya kusoma kwa kutumia laptop hizo na hii itakuwa ni nafasi kwao ya kuweza kujitunza zaidi.
"Kwa mara ya kwanza nilipokuwa nchini Tanzania nilipita Serengeti na kukuta mtu anajitahidi kutengeneza nyumba ambayo ni ngumu kuitengeneza hii inamaana kuwa mwalimu mmoja alikuwa anafundisha wanafunzi zaidi ya miamoja niliamua kuanzisha mahusiano na shule hiyo ambayo niliwapelekea vifaa mbalimbali vya kufundishia".
"Lengo la kuanzishwa kwa Taasisi hii ni kutoa msaada wa kielimu ikiwa na nia ya kufanya upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi kutoka nchi zinazoendelea ili wale wanaotoka katika familia maskini waweze kusoma na kupata ajira pale watakapokuwa wamemaliza masomo yao na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha", alisema Ricketts.
Alimalizia kwa kusema kuwa program zao za kufundishia wanafunzi zimeandaliwa kwa lugha ya kiingreza lakini hivi sasa wameanza kuandaa program hizo kwa njia ya Kiswahili jambo ambalo litazifanya shule ambazo zinafundisha kwa lugha hiyo nazo kunufaika na Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliishukuru taasisi hiyo kwa kusaidia kuboresha elimu nchini na kuiomba kuangalia uwezekano wa kuzifikia shule, walimu na wanafunzi waliopo vijijini ambao nao wanahitaji kupata njenzo nzuri za kufundishia na material mazuri ya kusoma kama ilivyo kwa wanafunzi wa mjini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeeo (WAMA) alisema kuwa kupitia taasisi hiyo ameweza kuwasaidia watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi ambao hawakupata nafasi ya kupata elimu kuwapatia ufadhili wa masomo na hivyo kuendelea na masomo yao.
Pia ameweza kuinua uchumi wa wanawake jambo ambalo limewafanya waweze kuimarisha hali zao za maisha kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali na kuwaongezea mitaji ya vikundi vyao vya maendeleo.
Mama Kikwete alisema, "Nakupongeza Bwana Ricketts kwa kazi unayoifanya ya kuzisaidia shule zaidi ya 400 nchini Tanzania msaada unaoutoa wa vifaa vya kufundishia unawafanya walimu waweze kufundisha masomo yao vizuri naamini tutajenga mahusiano mazuri kati ya Taasisi yako na WAMA ili kuhakikisha kuwa program hii inafanikiwa na kutimiza malengo yake".
Taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2005 na kusajiliwa nchini mwaka 2006 walianza kufanya kazi na shule moja ya msingi na hadi kufikia sasa shule 434 zikiwemo za Sekondari 33 zimenufaika kwa kupata vitabu, DVD na zana za kufundishia.
Kwa upande wa shule za sekondari wanatoa mwongozo wa mwalimu ambao unamuongoza kirahisi jinsi ya kuwafundisha wanafunzi , laptop ambazo zinamasomo yaliyorekodiwa ambayo ni ya sayansi, hesabu, kiingereza na maarifa ya jamii ,projecta na Televisheni ambazo zinasaidia kuonyesha masomo na vitabu na video inawasaidia wanafunzi kujifunza somo la kiingereza kwa njia ya kusikiliza na kusoma.
Mama Kikwete alipata nafasi ya kutembelea makao makuu ya Taasisi hiyo yaliyopo katika mji wa Omaha na kujionea nyenzo mbalimbali za kufundishia vikiwemo vitabu na DVD zikiwa zimefungwa kwa ajili ya kupelekwa katika nchi mbalimbali zinazoendelea za bara la Afrika na Asia ikiwemo Tanzania. Chanzo: Anna Nkinda – Maelezo, Lincoln

Chapisha Maoni

0 Maoni