Unordered List


CCM lazima Ichukue Dola kwa Kishindo 2015




Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga na kuendesha mafunzo kwa makatibu wake wa Mikoa na Wilaya zote hapa nchini. Mafunzo hayo pia yatajumuisha ushiriki wa wenyeviti wa wilaya na baadhi ya watendaji na watumishi wa Makao Makuu na ngazi nyingine zisizo rasmi za Chama Cha Mapinduzi.

Mafunzo hayo yameanza rasmi leo ambapo Makamu Mwenyekiti Taifa ambae pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein alifanya ufunguzi wa mafunzo hayo katika ukumbi wa Makao Makuu ya Chama maarufu kama whitehouse jijini Dodoma.


Katika Hotuba hiyo Makamu Mwenyekiti alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni vuguvugu za kuelekea 2014/2015 na kwamba watendaji wa chama watambue kuwa sasa wanaingia rasmi katika mbio na heka heka za Uchaguzi. Sehemu ya nukuu ya hotuba hiyo inasema


"..Napenda ieleweke kwamba, miongoni mwa malengo ya mafunzo haya ni kuimarisha uhai wa Chama chetu wakati huu tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara hapo mwakani pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.


Nina imani kubwa kuwa mafunzo haya yatakuwa na manufaa makubwa kwa washiriki wote na yataleta tija katika utendaji wa majukumu yenu. Tunategemea baada ya mafunzo haya, tutashuhudia na kuona vugu vugu la kuimarika kwa shughuli za chama chetu nchi nzima. Hali hiyo, lazima iende sambamba na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 ambapo kama kawaida yetu ushindi ni lazima.."

Pamoja na ufunguzi wa mafunzo, Makamu Mwenyekiti ameipongeza tume ya mabadiliko ya Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya na amebeza propaganda zilizoenezwa kuwa Chama Cha Mapinduzi kilihodhi mchakato wa ukusanyaji wa maoni na kwamba Chama Cha Mapinduzi kinawahakikishia watanzania kuwa kitaheshimu maoni ya watanzania wakati wa kura za maoni (referendum) wakati ukifika.

Katika kuhitimisha Dr Shein akahimiza Umoja ndani ya Chama na kuwakumbusha watendaji juu ya Uadilifu katika utendaji wao. Na kusisitiza kuwa Chama hakitashindwa kuwachukulia hatua wale wote wataogundulika kutokuwa na Uadilifu na kusababisha Uimara wa Chama kulega lega.

Chapisha Maoni

0 Maoni