BABA WA TAIFA AKIWA NA NELSON MANDELA ENZI ZA UHAI WAO
Familia ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere itawakilishwa
katika mazishi ya Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela, ambaye atazikwa kesho katika Kijiji cha Qunu, Mthatha Jimbo la
Eastern Cape.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata jana mjini Pretoria zinasema
kuwa Mama Maria Nyerere, ambaye ni mjane wa Baba wa taifa, alialikwa
kuhudhuria mazishi hayo kwa kuzingatia uhusiano uliopo baina ya familia
hizo mbili.
Hata hivyo, imethibitika kuwa Mama Maria hataweza kuhudhuria mazishi
hayo kesho, badala yake amewatuma wawakilishi ambao ni mabinti zake
wawili; Anna Nyerere ambaye ni mtoto wa pili na mtoto wake wa saba,
Rosemary Nyerere.
Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa sita wa Mwalimu alithibitisha
jana kwamba familia yao imealikwa kushiriki mazishi hayo, lakini akaweka
wazi kwamba: “Mama hataweza kwenda kuzika, atakwenda baadaye kidogo
baada ya mazishi kufanyika.”(P.T)
Madaraka alisema kwa jinsi afya ya mama yake ilivyo sasa, hataweza
kwenda Qunu. “Kwa kawaida mazishi haya ya kitaifa huwa yana mambo na
pilika nyingi, kwa hiyo mama ameona asubiri,” alisema.
Kuhusu kifo cha Mandela, Madaraka alisema kwamba kama wanafamilia,
wameguswa na msiba huo na kuwa kimewakumbusha uchungu walioupata wakati
walipofiwa na baba yao Oktoba 14, 1999.
“Kwa kweli tumeguswa sana na msiba na tunawapa pole sana, tunakumbuka
kwamba wakati baba alipofariki, Mama Graca tulikuwa naye, alikuja kabla
ya mazishi na alikuwepo kwenye mazishi na baada ya mazishi aliendelea
kukaa kwa siku kama saba,” alisema Madaraka na kuongeza:
“Pia tunakumbuka kwamba Mzee Mandela yeye alikuja baadaye mpaka
Butiama kutoa pole. Ilikuwa Novemba 26, 1999 kwa hiyo tunaguswa na msiba
huu.” Awali, gazeti hili lilidokezwa kwamba watoto hao wa Nyerere
walikuwa wamefikia katika Hoteli ya Burgers Park, Pretoria lakini
walipotafutwa katika hoteli hiyo wafanyakazi walisema kwamba tayari
walikuwa wameondoka.
Chanzo:Mwananchi
0 Maoni