Unordered List


KAMA ULIIKOSA MAANA YA HOTUBA YA OBAMA KWENYE MSIBA WA MANDELA,KWA SABABU YA KUTOJUA LUGHA YA KIINGEREZA BASI HII IMEJARIBU KIASI KUKUPA MAANA NA MWANGA ISOME;




Jumanne, Disemba 10, 2013

Kwa Graça Machel na familia ya Mandela;

kwa Rais Zuma na wajumbe wengine wa serikali;

kwa wakuu wa nchi na serikali, waliopita na waliopo sasa, wageni wengine waalikwa

– ni heshima ya kipekee mno kuwa nanyi leo, kusherehekea maisha yasiyo na kifani.

Kwa watu wa Afrika Kusini – watu wa kila rangi na kila mfumo wa maisha –

dunia inawashukuruni sana kwa kutushirikisha.

Nelson Mandela. Mapambano yake yalikuwa mapambano yenu.

Shangwe yake ikawa shangwe yenu.

Utu wenu na matumaini vilielezwa kupitia maisha yake, na uhuru wenu, na demokrasia yenu ni urithi wake uliotunzwa vema.

Ni vigumu kumsifu sana mtu yeyote –

kuweza kudaka maneno na siyo matendo na nyakati zilizoyafanya maisha yake, lakini kupata ukweli muhimu umhusuo

– furaha yake binafsi na huzuni; nyakati tulivu na ubora wa kipekee ulioiangaza nafsi ya mtu.

Ni ngumu mno kwa gwiji katika historia,

aliyelipeleka taifa katika haki, na katika mchakato uliowahuisha mabilioni ya watu ulimwenguni.

Aliyezaliwa wakati wa vita ya kwanza ya dunia, mbali kabisa kutoka mataifa yaliyokuwa na nguvu,

mvulana mdogo aliyekuwa akichunga ng'ombe na kufundishwa na wazee wake wa kabila lake la Thembu

– Madiba aliweza kuibuka kama mkombozi wa mwisho wa karne ya 20.

Kama ilivyokuwa Ghandhi, aliongoza mapambano

– harakati ambazo mwanzo wake ulionesha nuru ndogo ya mafanikio.

Kama King, alipaza sauti yake ya manung'uniko ya wanaokandamizwa,

na uadilifu muhimu wa haki kwa kila rangi.

Alipambana na kifungo cha kikatili kilichoanza wakati wa Kennedy na Khrushchev,

kilichokwenda hadi nyakati za mwisho za Vita Baridi.

Aliibuka kutoka jela, pasipo kutumia nguvu ya bunduki,

akaweza – kama Lincoln – kuileta nchi yake pamoja ilipokuwa katika hatari ya kuvunjika vipandevipande.

Kama waasisi wa Amerika, aliweka misingi ya kikatiba ya kuhifadhi uhuru kwa ajili ya vizazi vijavyo

– kujitolea kwa ajili ya demokrasia na utawala wa sheria ulioridhiwa si tu na uchaguzi uliomweka madarakani bali na hiyari yake ya kuachia madaraka.(P.T)

Kwa kuondoka kwake, na kwa mapenzi aliyoyapata akiyastahili,

inashawishi kumkumbuka kama alama, yenye tabasamu na iliyotakata,

iliyojiepusha na maovu ya wengine wasio na utu.

Lakini Madiba mwenyewe alikataa kwa nguvu zote taswira isiyo na maana.

Badala yake, alisisitiza katika kushiriki nasi mashaka yake na hofu yake;

makosa yake sambamba na kushinda kwake.

"Mimi si mtakatifu," alisema, "
I
sipokuwa kama mnanidhania mtakatifu mwenye dhambi asiyeacha kujaribu."

Ni kwa sababu tu alikubali kuwa na mapungufu

– kwa kuwa alijaa ucheshi, hata kukosea, licha ya mizigo mizito aliyokuwa ameibeba

– nasi tukampenda vivyo hivyo.

Hakuwa mtu aliyetengenezwa kwa marumaru;

alikuwa binadamu wa kawaida

– mtoto na mume, baba na rafiki.

Hayo yote yanaonesha ni kwa nini tumejifunza mengi sana kutoka kwake;

na ndiyo sababu bado tuna mengi ya kujifunza kutoka kwake.

Kila alichokipata hakikuepukika.

Katika utao wa maisha yake, tunamwona mtu aliyeiweka nafasi yake kwenye historia kwa kupitia mapambano na werevu;

msimamo na imani.

Ametuambia nini kinachowezekana si tu kwa kupitia kurasa zenye vumbi za vitabu vya historia,

bali pia kwa kupitia maisha yetu wenyewe.

Mandela ametuonesha nguvu ya matendo,

kukabiliana na hatari kwa ajili ya ukamilifu wetu.

Pengine, Madiba alikuwa sahihi kusema amerithi,

"ukaidi wa kujivunia, utukutu katika haki"

kutoka kwa baba yake.

Kwa yakini ameshiriki na mamilioni ya Waafrika Kusini weusi na wengine wa rangi mchanganyiko hasira ya kuzaliwa katika

"maelfu ya twezo, maelfu ya vitendo vilivyokosa utu, maelfu ya nyakati zisizokumbukika.....matamanio ya kupambana na mfumo uliowafunga watu wangu".

Lakini kama manguli wengine wa ANC – akina Sisulu na akina Tambo

– Madiba alikuwa na nidhamu ya hasira yake;

akayapeleka matamanio yake ya mapambano kitaasisi, na katika ulingo,

na kwa mikakati mahsusi, kwamba waume na wake wangeweza kusimama kwa ajili ya utu wao.

Vilevile, akayakubali madhara ya matendo yake, akifahamu kuwa kusimamia haki na usawa kuna gharama zake.

"Nimepambana dhidi ya ukandamizaji wa watu weupe na nimepambana dhidi ya ukandamizaji wa watu weusi,"

aliyasema hayo katika kesi yake ya mwaka 1964.

"Nimeutukuza ukamilifu wa demokrasia na jamii huru ambapo watu wote huishi kwa pamoja katika maelewano na fursa sawa.

Ni imani ninayoishi nayo nikitumaini kuipata.

Lakini ikihitajika, ni imani niliyojiandaa kuifia."

Mandela ametufundisha nguvu ya matendo,

lakini pia mawazo; umuhimu wa kuwa na sababu na hoja;

umuhimu wa kuwasoma siyo tu wale unaokubaliana nao,

bali pia wale usiokubaliana nao.

Alifahamu mawazo hayawezi kuhifadhiwa ndani ya kuta za jela,

ama kuondoshwa kwa risasi ya mdunguaji.

Akaigeuza kesi yake kuwa mashitaka rasmi dhidi ya ubaguzi wa rangi kwa kupitia uzungumzaji wake na hisia kali,

pia kwa kupitia mafunzo yake kama wakili.

Akaitumia miongo ndani ya jela kunoa uwezo wake wa kujenga hoja,

lakini pia kueneza kiu yake ya maarifa kwa wengine katika harakati za mapambano.

Akajifunza lugha na tamaduni za wakandamizaji wake ili siku moja aweze kuwaonesha ni kwa kiasi gani uhuru wao ulitegemea pia uhuru wake.

Mandela alionesha kuwa matendo na mawazo pekee havitoshelezi;

haijalishi ni sahihi kwa kiasi gani,

vinatakiwa kuwa kisheria na kitaasisi.

Alikuwa mtu wa vitendo, akazijaribu imani zake dhidi ya mazingira magumu na historia iliyokuwepo.

Katika kanuni ya msingi hakukubali kushindwa,

hicho kilipelekea akatae kuachiwa huru kwa masharti,

akiukumbusha utawala wa kibaguzi kuwa,

"kamwe mfungwa haingii katika mikataba".

Lakini alionesha katika majadiliano magumu nia ya kupeana madaraka na kuandika sheria mpya,

hakuogopa kufikia maridhiano kwa malengo makubwa.

Na kwa kuwa hakuwa pekee yake kama kiongozi wa harakati,

lakini akiwa mwanasiasa mweledi,

katiba iliyoandikwa ikawa yenye kuthamini demorasia ya rangi tofauti;

ikiweka bayana maono yake juu ya sheria inayolinda haki za wachache na za wengi pia,

na uhuru wa tunu kwa kila Mwafrika Kusini.

Hatimaye, Mandela alielewa juu ya mambo yanayoiunganisha roho ya mwanadamu.

Kuna neno Afrika Kusini – Ubuntu – linaloelezea hiba yake kubwa:

kutambua kwake kuwa sisi sote tunaunganishwa katika namna mbalimbali ambazo zinaweza kutoonekana kwa macho;

ambazo zinaonesha u-moja kwa binadamu;

kwamba tunakuwa sisi kwa kushirikisha wengine katika u-sisi, na kuwajali wale wengine wanaotuzunguka.

Hatuwezi kufahamu ni kwa kiwango gani hii ilikuwa ndani yake, ama kwa kiasi gani ilichochewa na kung'arishwa katika selo yenye kiza na upweke.

Lakini tunakumbuka ishara ya mwili wake, kwa ukubwa na udogo wake –

akiwatambulisha mabwana jela wake kama wageni wa heshima siku aliyoapishwa;

ndani ya sare ya Springbok; akiigeukia familia yake akiihamasisha kupambana na VVU/UKIMWI

– ikionesha kiwango cha juu cha huruma yake na uelewa.

Si tu alikolezwa na Ubuntu;

bali aliwafundisha wengi kuitafuta kweli ndani yao.

Ilimchukua mtu kama Madiba kumkomboa si tu mfungwa, bali na bwana jela pia;

kuonesha kuwa unapaswa kuwaamini wengine ili nao waweze kukuamini wewe;

kufundisha kuwa maridhiano hayamaanishi kuyadharau machungu yaliyopita,

bali kumaanisha kupambana nayo kwa ushirikishaji,

ukarimu na ukweli. Alizibadili sheria, lakini na mioyo pia.

Kwa watu wa Afrika Kusini, kwa wale wote aliowapa msukumo kote ulimwenguni

– kufariki kwa Madiba ni wakati hasa wa maombolezo, na pia wakati wa kuyasherehekea maisha yake ya kishujaa.

Lakini ninaamini inapaswa pia kutupa wasaa wa kujitathimini wenyewe.

Kwa uaminifu, pasipo kujali mahali tulipo ama hali tulizo nazo, shurti tujiulize:

kwa namna gani ninayatekeleza mafunzo yake kwenye maisha yangu
mwenyewe?

Ni swali ninalojiuliza mwenyewe

– kama binadamu na kama rais.

Tunafahamu kama ilivyo Afrika Kusini, Amerika ililazimika kupambana na karne za ubaguzi wa rangi.

Kama ukweli ulivyo hapa, iliwachukua watu wasiohesabika kujitoa mhanga –

wanaojulikana na wasiojulikana – kuleta mapambazuko ya siku mpya.

Michelle pamoja nami ni wanufaishwa wa mapambano hayo.

Lakini ndani ya Amerika na Afrika Kusini, na nchi zingine kote ulimwenguni,

hatuwezi kuruhusu maendeleo yetu kuufunika ukweli kuwa kazi yetu haijafanywa.

Mapambano yanayofuatia ushindi juu ya usawa na haki za kiraia kote ulimwenguni yanaweza yasitoshelezwe uadilifu na unyoofu ukilinganisha na yale yaliyotangulia,

lakini haimaanishi umuhimu kidogo.

Kwa dunia ya leo, tungali tukiwaona watoto wakiteswa na njaa,

na magonjwa; kukosa shule, na matarajio yao machache kwa maisha ya baadaye.

Duniani kote leo, wake na waume wangali wakifungwa kwa ajili ya imani zao kisiasa;

na wangali wakiadhibiwa kwa vile waonekanavyo,

ama vile waabuduvyo, ama nani wawapendao.

Sisi, pia, lazima tutende kwa ajili ya haki.

Sisi, pia, lazima tutende kwa ajili ya amani.

Wapo wengi mno miongoni mwetu ambao kwa furaha tunaukumbatia urithi wa Madiba katika maridhiano ya rangi,

lakini kwa hisia kali tunayakataa mabadiliko ya wastani ambayo yangeshindana na umasikini sugu na kukosekana kwa usawa kunakokua.

Wapo viongozi wengi mno wanaodai kushikamana na mapambano ya uhuru ya Madiba,

ilhali hawavumilii maoni tofauti kutoka kwa watu wao wenyewe.

Na wapo wengi wetu wanaosimama pembeni, wakistarehe katika kuridhika ama wakizidharau sauti zetu zinapolazimika kusikika.

Maswali tunayokumbana nayo leo –

tukuze vipi usawa na haki;

tuulinde vipi uhuru na haki za kibinadamu;

tukomeshe vipi migogoro na vita vya wenyewe

– hayana majibu rahisi.

Lakini hakukuwa na majibu rahisi mbele ya mtoto yule pale Qunu.

Nelson Mandela anatukumbusha kuwa daima huonekana haiwezekani hadi jambo linapotendwa.

Afrika Kusini inatuonesha kuwa hivyo ni kweli.

Afrika Kusini inatuonesha tunaweza kubadilika.

Tunaweza kuchagua kuishi katika dunia isiyotafsiriwa kwa tofauti zetu,

bali kwa matumaini yetu yanayofanana.

Tunaweza kuichagua dunia isiyotafsiriwa kwa mgogoro,

bali kwa amani na haki na fursa.

Hatutowaona watu kama Nelson Mandela tena.

Lakini wacha mimi niseme kwa vijana wadogo wa Afrika,

na vijana wadogo kote ulimwenguni

– mnaweza kuyafanya maisha yake yakafanya kazi ndani yenu.

Zaidi ya miaka thelathini iliyopita,

nikiwa bado mwanafunzi, nilijifunza kuhusu Mandela na mapambano katika nchi yake.

Ilichochea kitu ndani yangu.

Iliniamsha katika wajibu wangu – kwa wengine, na kwa nafsi yangu -

- na kuniweka katika safari isiyoyumkinika ambayo imenifikisha hapa leo.

Na wakati sitoufikia mfano wa Madiba, ananifanya nitake kuwa bora.

Anazungumza kilicho bora ndani yetu.

Baada ya huyu mkombozi mufti kupumzishwa;

baada ya sisi kurudi kwenye majiji yetu na vijiji vyetu,

na kurejea mizunguko yetu ya kila siku,

ni vema tuitafute nguvu yake
– kwa ukuu wa roho yake

– mahali fulani ndani yetu.

Na wakati giza likiingia usiku,

wakati ukosefu wa haki ukituelemea mioyoni mwetu,

mikakati yetu kutofanikiwa –
tumfikirie Madiba,

na maneno yaliyomletea faraja ndani ya kuta nne za selo yake:

Haijalishi namna mashaka yalivyoniandama,

Namna nilivyoshtakiwa na adhabu ndefu,

Mimi ndiye mwamuzi wa majaaliwa yangu,

Mimi ndiye nahodha wa nafsi yangu.

Ni nafsi kuu kwa kiasi gani.

Tutamkumbuka juu mno.

Mwenyezi Mungu aibariki kumbukumbu ya Nelson Mandela.

Mwenyezi Mungu awabariki watu wa Afrika Kusini.

Chapisha Maoni

0 Maoni