Na. Zainul Mzige
Ingawaje
Tanzania inaitwa nchi masikini pamoja na kwamba wahisani na wadau wa
maendeleo wanasema ni nchi inayoendelea lakini kwa ujumla na kwa yeyote
anayeijua nchi yetu kwa maana ya hali ya maisha ya wananchi wake, ni
jambo la hatari kwa kikundi kidogo cha watu waliokalia ofisi za umma na
kujipangia utaratibu fulani wa kujinufaisha.
Kikundi
hiki kidogo tena kilichochaguliwa na wananchi kama wawakilishi wao
(wabunge) na ndio watunga sheria kujinufaisha kwa jasho la walipa kodi
kwa kisingizio cha sheria ambazo wametunga wao wenyewe kwa kujipendelea.
Ni
aibu zaidi kusikia kwamba wabunge wengi na hata baadhi ya mawaziri
kukejeli juhudi binafsi za baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania wenye kuogopa kodi za wananchi na kutaka mabilioni
hayo kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi kwa maslahi
mapana ya taifa.
Tumeamua
kusema hayo bila kuficha kwamba ni muhimu kwa Serikali pamoja na Bunge
kufikiri upya mtindo huu wa kifisadi wa kulipana posho ya kukaa (Sitting
Allowance) wakati wana mishahara mikubwa kuzidi wafanyakazi wenye
kufanya kazi usiku na mchana kama vile madaktari wanaosubiri kulipwa
posho ya (overtime) ya shilingi elfu kumi ambayo hukaa hadi miezi mitatu
mpaka sita haijalipwa.
Tunasema
na kusisitiza kuwa ujira wa vikao ambavyo ni kazi halali za ubunge ni
mshahara na si posho! Posho ni wizi wa fedha za umma mchana kweupe kwa
sababu kazi ya Mbunge ni uwakilishi na pale anapokaa kwenye vikao vya
bunge na kamati mbalimbali anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na
katiba ya nchi iweje alipwe Posho?
Mwaka
juzi kwenda mwaka jana 2011/2012 Serikali ililiomba Bunge kupitisha sh
bilioni 987 kwa ajili ya psoho mbalimbali za watumishi wa Serikali
wakiwamo wabunge. Hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa changa kama
Tanzania.
Huu
ni kweli kwamba mabilioni ya shilingi zikiwa ni kodi za wananchi kila
mwaka wa fedha yanatengwa kwa ajili ya posho tu, na hata mwaka jana
Benki ya Dunia na wahisani wa maendeleo walihoji uwepo wa posho za kukaa
kwa watumishi wa serikali na wabunge lakini bado tatizo hili la kuzoea
posho linaitafuna nchi yetu bila huruma.
Serikali
kupitia wizara ya fedha mwaka 2011/2012 iliahidi kwamba posho ambazo
hazina tija zitaondolewa kauli iliyoonekana kama mwanzo wa mageuzi ya
kweli, lakini leo asubuhi niliposikia kipindi cha tuongee magazeti juu
ya Wabunge kutafuna posho ovyo wote wa chama tawala na upinzani ni
ishara kwamba serikali ilitaka kauli ile ieleweke kinyume nyume.
Gazeti
la kila wiki la Raia Mwema limeongoza leo na habari za wabunge kutafuna
posho hovyo hovyo na Mbunge kijana Joshua Nasari amekiri kwamba
alichukua posho ya kwenda safari Malaysia lakini ikatokea dharula ya
Harambee jimboni kwake akaona ni busara kujumuika na wananchi wake bravo
kwake.
Bila
kutafuna maneno Tanzania ni nchi maskini, kwani kipato cha mwaka cha
mwananchi wa kawaida ni Sh 770,463 hivi, wastani wa kama Sh 2,140 kwa
siku, kwa mantiki hiyo Mtanzania wa kawaida kuishi katika maisha ya leo
kwa kipato hiko ni kwa kudra za mwenyezi mungu kama si rushwa dogo dogo
zinazomwezesha kumaliza mwaka.
Lakini
wakati wananchi walio wengi wakiishi katika umaskini wa kutupa, wapo
watu waliaomua kusaka nafasi za uongozi katika nchi hii si kwa nia ya
kusaidiana na wananchi kutokomeza umaskini ulioelemea taifa hili, ila
kujitenga nao kwa kutengeneza utaratibu mbaya na kandamizi wa kujilipa
mafao manono kama hizi zinazoitwa posho za vikao za wabunge.
Kwa
maelezo yoyote yale, posho hizi si halali hasa zinapolipwa na taifa
maskini kama Tanzania ambalo haliwezi hata kujitegemea kwa kuwa na
bajeti yake walau kwa mwaka mmoja tu bila kutembeza bakuli kwa wafadhili
ili kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa
mtanzania yeyote makini atakubaliana nasi kwamba walioweka utaratibu
huu ama walipotea njia kwa ama walitanguliza mbele maslahi binafsi
lakini wananchi wameamka na wanajua kinachoendelea na wanawasubiri 2015
kwenye uchaguzi watawaita wabunge wa posho na vitambi vya posho kama si
mchemsho na kiti moto na bia kaeni chonjo uchaguzi unakuja!
Na
kuna taarifa za kutisha kwamba siku hizi hata kazi ambazo ni wajibu wa
watumishi wa umma kuzifanya watu hawafanyi mpaka kuwepo na posho
(Bahasha) yaani ofisa wa serikali kukaa kwenye kikao cha kazi ambayo ni
wajibu wake, anadai mshiko tumekwisha!
Kwa
utaratibu huu watanzania itatuchukua muda mrefu mpaka kuja kupata
maendeleo ya kweli na hakuna jambo lolote linalokwamisha uwezo wa
serikali kutimiza wajibu wake zaidi ya maposho yasiyo kuwa na kichwa
wala miguu ndugu zangu tukafanye kazi tuliotumwa na wananchi tuache
rongo rongo za posho zisizo kuwa na tija kwa maslahi ya vizazi vya sasa
na vijavyo.
Naomba kuwasilisha !
0 Maoni