Unordered List


SERIKALI YATOA TAMKO KUHUSU KUSITISHA UTARATIBU WA KUKODISHA WAFANYAKAZI UNAOFANYWA NA BAADHI YA WAKALA BINAFSI WA HUDUMA ZA AJIRA


Waziri wa Kazi na Ajira Bi.Gaudentia Kabaka akitoa tamko la Serikali kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya usitishwaji wa utaratibu wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya mawakala binafsi wa huduma za ajira wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa idara ya habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.
*****************************
TAMKO LENYEWE HILI HAPA
1. Wizara ya Kazi na Ajira imekua ikipokea malalamiko  toka kwa wadau mbalimbali kuhusu taratibu wa udalali wa kukodisha wafanyakazi katika makampuni unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini.

2. Wizara imefanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na kubaini kuwa utaratibu wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya Mwaka 1999  (Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002). Kwa mujibu wa Kifungu 4 cha Sheria hii, majukumu ya msingi ya Wakala wa Huduma za Ajira ni kuwaandaa na kuwaunganisha Watafuta Kazi na Waajiri kwa kutoa mafunzo na  ushauri elekezi kwa watafuta kazi,  kutafuta fursa za ajira na kutoa taarifa za soko la ajira.  Hivyo, Mawakala hawapaswi kuwa waajiri wa wafanyakazi waliowatafutia kazi kwa niaba ya Waajiri wengine.

3. Aidha, uchunguzi umebaini kwamba  utaratibu huu ni ujanja unaotumiwa na baadhi ya Waajiri na Mawakala kwa lengo la kukwepa kodi na kujipatia faida kwa kukwepa kutoa haki za msingi za wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za Kazi. Baadhi ya makampuni yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa uhakiki na TRA na kubainika kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na  na kodi ya mapato ya kampuni kinyume na Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004 (Sura 332 kama ilivyorejewa Mwaka 2008).

4. Uchunguzi huu umebaini  athari mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huu. Athari hizo ni pamoja na:
· Wafanyakazi kukosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na matibabu kinyume na Sheria mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
· Uwepo wa ubaguzi katika malipo ya mishahara kwa kazi ya aina moja kinyume  na  kifungu cha 7(10) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004 ambacho kinamtaka mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kuwa wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa mishahara linganifu na ya haki kwa kazi yenye uzito na thamani sawa;
· Kukosa fursa za kujiendeleza kielimu na mafunzo;
· Kukosekana kwa usalama na uhakika wa ajira ;
· Wafanyakazi kulipwa mishahara ya kima cha chini kinyume na sekta wanayofanyia kazi.

5. Kwa taarifa hii, Wizara ya Kazi na Ajira imeamua kusitisha mara moja utaratibu wa Mawakala kuwaajiri  wafanyakazi wanaowatafutia kazi.  Aidha, Mawakala na Kampuni husika waliopo katika utaratibu huu kwa sasa wanapaswa kuwahamisha  wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwa Wakala kwenda  kwa Kampuni husika. Waajiri na Wakala wanatakiwa kukamilisha zoezi hili ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kabla au ifikapo tarehe 28/02/2014.

6. Uchunguzi zaidi unaendelea kubaini kama kuna wafanyakazi wa Kigeni wanaohusishwa katika utaratibu wa kukodishwa ili hatua zinazotahili ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwataka waombe vibali vya ajira kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995 na Sheria ya Huduma za Ajira Na.9 ya mwaka 1999. Wageni watakao kidhi vigezo wataajiriwa na kampuni walipokodishwa; ambazo kwa wakati huo zitakua ndiyo mwajiri wao.

7. Wizara ya Kazi na Ajira inawaelekeza Wakala wa Huduma za Ajira nchini kwamba, kwa utaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za maombi ya  usajili wa Uwakala kwa KAMISHNA WA KAZI  kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002] ili waweze kufanya shughuli za Uwakala wa Huduma za Ajira kisheria. Maombi haya yawasilishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kutolewa kwa tangazo hili. Baada ya muda huo Wakala asiye na kibali cha Kamishna wa Kazi hatoruhusiwa kuendesha shuguli za huduma za ajira nchini. Aidha, Mawakala watakaopata leseni ya Kamishna wa Kazi yatakua yakitangazwa ili yatambuliwe na Umma.

8. Nasisitiza, maelekezo haya yatatolewa kwa Makampuni na Wakala  waliohusishwa katika uchunguzi kwa ajili ya utekelezaji.

IMETOLEWA NA
GAUDENTIA MUGOSI KABAKA (MB)
WAZIRI WA KAZI NA AJIRA
27/01/2014se

Chapisha Maoni

0 Maoni