MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
SALAMU
ZA PONGEZI KWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE
Utangulizi:
Ndugu waandishi wa
habari, mabibi na mabwana. Leo tena nimewaita kwa ajili ya kuzungumza mambo
machache muhimu yahusuyo taifa letu Tanzania.
Yangu leo ni machache
na muhimu ni kutoa salamu za pongezi za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba murua aliyoitoa Juzi 21/03/2014 wakati akizindua bunge
maalum la katiba. Kama taasisi muhimu katika taifa hili, tumechukua hatua hii
madhubuti kulieleza taifa umuhimu wa ile hotuba, mantiki iliyopo katika ile
hotuba, na kwa kuwa sisi tunawakilisha sauti za vijana zaidi ya milioni 25 wa taifa hili, na kwa kuwa
athari nyingi za katiba hii tunayotengeneza zitawaathiri sana vijana kuanzia
sasa na mustakabali wao. Hatuwezi kukaa kimya ama tukaungana na wale wenye
kulaumu pasipo kujua mantiki, maana mwisho wa siku vijana hawatawalaumu wale
wanaowapotosha kwa sauti zao kali, bali watawalaumu wale walio na ufahamu na
wakakaa kimya kama Martin Luther "King" alivyowahi kusema;
"In The End we
will remember, Not the Voices of Our Enemies, but The Silence of Our
Friends".
Sisi ni rafiki wa
Taifa hili na watu wake, hatuwezi kukaa kimya huku tukiwaona wale wasitutakia
mema wakiendelea kueneza sumu mbaya ya kutugawa katika makundi makundi.
Ndugu waandishi,
Tanzania ina watu milioni 49 (kwa
takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na makadirio yake ya mwaka
2013). Kwa kuwa bunge hili maalum limechukua mfumo wa uwakilishi wa watu wote
kwa makundi yao (yaani fair representation),
kwa bunge lenye wajumbe 619, maana
yake ni kuwa, kwa wastani kila Mbunge anawakilisha Watanzania 79,000. Sasa hapa ndipo kwenye kazi na mantiki
tunayoijenga; kwamba
i.
Ikiwa Mbunge mmoja atasimama bungeni
na kutekeleza wajibu wake ipasavyo, basi sauti za watanzania 79,000 zitakuwa zimewakilishwa vema, na akifanya tofauti
yake halikadhalika haohao watanzania kwa hasara yao.
ii.
Fikiria kwa mfano Mbunge akasimama
dakika tano akatumia muda huo kutukana badala ya kujenga hoja kwa manufaa ya
taifa, maana yake ni kuwa hawa watanzania elfu
79 wamepoteza dakika 79000x5=4,345,000
ambayo ni sawa masaa 72,461 ama siku 3,071 ambayo kimahesabu ni karibu
miaka kumi. Hebu fikiria huyu ni Mbunge wako yaani kwa kitendo cha dakika tano
amekufanya umepoteza miaka 10 kwa
kutukana mfululizo.
iii. Ikiwa
Mbunge atatumia hizo dakika tano, badala ya kujenga hoja zenye maslahi ya taifa
na badala yake ajenge hoja ya ama chama chake cha siasa ama kundi
lililompeleka, ama kwa kushawishiwa na mwingine ambaye anataka kutimiza matakwa
yake, basi Raia ambaye anawakilishwa na huyu mtu, ni sawa na kwamba ameishi
miaka kumi katika uso wa dunia hii bila malengo.
Ndugu waandishi,
hesabu hizo hapo kwa udhahania wake zina maana tu kama wabunge wote wa bunge
hili watathamini nafasi zao kama ni tunu kwa ustawi wa taifa na si ustawi wa
ama wao binafsi ama taasisi zao, ama vyama vyao vya siasa ama madhehebu ama
kitu kingine chochote. Yale ambayo mheshimiwa Rais amewaasa wabunge na wanachi
kwa ujumla ni kuhakikisha kuwa wanajiridhisha na mwenendo mzima kutoka mwanzo
wa mchakato hadi tutakapofika mwisho wa mchakato huu na kupata katiba mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Umuhimu wa hotuba ya
rais kwa upande wetu UVCCM tumechukua mambo mawili muhimu 1. Rais Kutupitisha
katika Historia muhimu ya taifa letu
kuhusu Katiba, Muungano, Masuala mengine ya Muungano na Michakato ya maamuzi ya
masuala yahusuyo utawala wa taifa letu; na 2. Umuhimu wa kutumia historia ya
kila jambo wakati wa kufanya maamuzi yahusuyo jambo hilo;
1. Kutupitisha katika
Historia ya Taifa
Kwanza tuseme wazi,
vijana wa CCM tumeridhika pasi na shaka kwa mtindo ambao Rais aliutumia
kuwaeleza wabunge na watanzania kwa kina ufanisi na kwa lugha inayoeleweka
kirahisi historia ya michakato mbalimbali tuliyopitia kama katiba, tangu mwaka
wa uhuru wa iliyokuwa Tanganyika (Tanzania Bara) na Zanzibar. Mabadiliko
makubwa ya katiba ya nchi hizi mbili ya mwaka 1965 na yale ya mwaka 1977.
Marekebisho mengi ya katiba yamefanyika kati ya mwaka 1977 na 2013/14.
Marekebisho yote yalihusu utashi wa serikali zote mbili (ya jamhuri na ile ya
Zanzibar) katika azma ya kufikia mafanikio ya kujenga taifa lililo na heshima,
lenye kuheshimu misingi ya utawala wa kidemokrasia, sheria na haki. Historia
hujenga ama hubomoa taifa. Hakuna ujenzi wa taifa bila kujua historia ya taifa
husika. Kuijua historia yetu si tu kwamba inatupa nafasi ya kujisikia na
kujivuna watanzanaia, bali inatupa naafasi ya kuwa na fikra pevu zaidi, juu ya
hatua gani tuchukue kuendelea kuijenga Tanzania yetu katika mshikamano, umoja
na udugu ikiwa kazi kubwa waliyoweza kuifanya waasisi wetu.
Leo hii kitendo cha
baadhi ya watu kuwabeza waasisi wetu, ni kubeza historia yetu, na kitendo cha
kulibeza taifa letu. Sababu bila juhudi zao na kutokuwa kwao wabinafsi, leo tunaishi
kama familia moja. Anayedharaua historia yetu, na asiyetaka kujifunza kutoka
kwa waliotutangulia, huyo ni mtumwa.
Katika idadi ya watu milioni 49, tuliopo, asilimia 44.8% (ambao ni karibu milion 22 ni watoto chini ya miaka 15
na asilimia 62.3% (ambao takribani
watu milion 31) wana umri chini ya miaka 25. Ukienda mbele kidogo kwenye
takwimu, utakuta kwamba asilimia 92.3%
ya watanzania wanaishi kwa utegemezi, yaani maana yake takribani watu milioni 45 wa taifa hili ni wategemezi
si wazalishaji na kwamba wazalishaji ni milioni nne tu. Na hii inatokana,
kwanza na ile asilimia 44.8% ya
watoto na kwa kiwango kikubwa asilimia
64% ya vijana walio chini ya miaka
25 kwa maana kwa taifa letu, kijana wa miaka
25 bado si mzalishaji maana ama bado anawategemea wazazi wake, ama bado
yupo shule. Takwimu hizi pia zaonyesha, wastani wa umri wa watanzania ni miaka 17, umri wa juu wa Mtanzania
kutegemea kuishi umekadiriwa kuwa ni miaka
60. Tanzania na takwimu kama hizi, lazima wajifunze na kuelewa kwa undani
mambo yahusuyo taifa.
Kuijua Historia ya
nchi yako, kuwa na ufahamu wa takwimu muhimu zihusuzo uchumi na idadi ya watu
na makazi, inakupa mwanga bora wa kutengeneza sera, kanuni na sheria
zitakazolinda mustakabali wa taifa lako na ustawi wake. Fikiria kwa mfano
karibu nusu ya watanzania wana umri wa chini ya miaka 15, halafu wastani wa umri wa watanzania ni miaka 17, wakati huo huo sheria za nchi
zinasema wale wanaoweza kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi ni wenye umri
kuanzia miaka 18, je unafanya nini
kutengeneza sera zitakazobeba masuala haya kwa pamoja. Badala ya kutumia nguvu
kutaka kulazimisha mambo fulani ambayo watu kama viongozi wanayataka, ni vema
tukaijua historia, tukajua mahitaji muhimu kwa sasa na wakati ujao ndipo
tutaweza kufikia kutengeneza taifa lenye uchumi endelevu unaostawi na kuwa
mfano kwa Afrika na duni kwa ujumla.
Sisi UVCCM tumeamua
kulisemea hili kwa uwazi na kwa sauti pana ili kuujuza umma wa watanzania
kwamba wawapuuze wale wote wanaotaka kuwaondoa katika mchakato huu muhimu na
kuwapeleka kule wasikotaka. Tunatambua nia njema ya serikali ya Chama Cha
Mapinduzi na dhamira ya dhati kuhakikisha tunapata katiba Mpya. Na sote
tunatambua kuwa kama serikali isingekuwa na nia njema, basi Tume maalum ya
Katiba isingeundwa, au ingeundwa lakini isingejihusisha na ukusanyaji wa maoni
nchi nzima. Na ikumbukwe, mchakato huu umepitia changamoto nyingi sana. Pamoja
na changamoto hizozilizokuwa na kila sababu ya kukwamisha zoezi la mchakato wa
katiba hii, Rais wetu kipenzi alisimama imara na kuhakikisha anatatua
changamoto zote hizo ili kutimiza adhima na ndoto za watanzania kupata katiba
mpya. Tunathamini kwa asilimia 100%
kazi iliyofanywa na tume chini ya Uenyekiti wa Jaji J.S. Warioba. Wapo ambao badala ya kujikita na maana halisi ya
kazi hizi na hotuba za viongozi hawa, wao wanajihusisha na kutafuta umaarufu wa
kisiasa kwa lengo la kujikusanyia wafuasi pasipo kutazama kwa kina zaidi
mahitaji ya watanzania ya sasa na kila changamoto ya muundo wa serikali kwa
siku zijazo. Na ndiyo maana Rais akiwa mkuu wa nchi ametoa taswira pana zaidi
ya kule tulikotoka, tulipo na kule tuendako, na kuwataka wabunge wapime kila
hoja na kila muunda wa serikali ili kuipatia Tanzania na Katiba
inayotekelezeka. Cha ajabu, wapo walioanza kujipanga kuanza kuharibu dhana zima
iliyoko katika dhamira ya viongozi wa taifa hili. Hizi ni hila mbaya ambazo
hazikubaliki katika taifa la watu waliostaarabika Tanzania.
Kitendo cha Rais
kutoa historia ndefu ya kule tulikoanzia na tulipo kuhsiana na katiba,
muungano, Afrika Mashariki, masuala ya muungano, Mahusiano ya Zanzibar na
Tanzania bara, kwanza inatoa morali kwa vijana na watoto kutamani kujifunza
zaidi, inatoa wajibu kwa wabunge kujisomea zaidi na kuja na uelewa mzuri wa
masuala yote yahusuyo taifa. Ametoa wajibu kwa maneno ya wazi kabisa;
"Akili ya
kuambiwa, Changanya na ya Kwako"
Sisi tunaweka
changamoto hapa, Ili uweze kuchanganya na ya kwako, sharti uwe nayo. Na namna
pekee ya kuwa nayo, ni kusoma rasimu ya katiba kwa bidii, sura kwa sura, sehemu
kwa sehemu, ibara kwa ibara, msitari kwa msitari, neno kwa neno na nukta kwa
nukta. Si kukaa na kusubiri tu nani aseme ili ama uzomee ama upige makofi.
Rais Kikwete kwa
matukio mawili ameiweka nchi kwenye ramani ya ulimwengu kuwa ni taifa ambalo
linafanya mambo yake kwa utaratibu wa kisheria unaokubalika kimantiki na kwa
utaratibu ambao hauleti migogoro na pale kunapotokea migongano, kumekuwa na
njia muafaka za kuimaliza. Alifanya hivyo kule Afrika kusini kwenye maziko ya mwanamapinduzi
halisi wa Afrika Hayati Nelson Mandela Madiba na amefanya hivyo Juzi Dodoma.
Huu ndio ukweli, kama kuna ambaye hataki aje na hoja si kuja na ubishi usio na
maana.
2. Umuhimu wa kutumia
Historia katika kufanya maamuzi
Watanzania wachache
sana walijua mahusiano yaliyokuwepo kati ya masuala yahusuyo muungano na uwepo kabla
wa jumuiya ya afrika Mashariki na baadaye uvunjifu wake mwaka 1977. Taifa kwa
miaka yote limepitia kwanza historia ya masuala hayo kabla ya kufanya maamuzi.
Hata muundo wa Bunge maalum la katiba umezingatia hali halisi ya sasa, uhitaji
mkubwa wa watanzania kutaka katiba, ongezeko la mikataba ya kimataifa ambayo
Tanzania imeridhia na hata kutengeneza katiba inayohusisha angalau uwakilishi
wa watanzania wote (fair representation).
Itoshe kukubaliana
kwamba, endapo wabunge wa bunge maalum la katiba watajipa muda mwingi wa
kujisomea tafiti mbalimbali, historia ya taifa hili na mataifa mengine mengi
duniani yaliyofikia hatua kama tunayoiendea, tukasoma vizuri rasimu ya katiba
pamoja na ripoti ya Tume ya Warioba pamoja na ripoti mbalimbali za zamani
zilizopelekea marekebisho ya katiba ya mara kwa mara (toka mwaka 1977), basi ni imani ya sisi vijana kwamba, tutatoka na
rasimu nzuri ya katiba, si tu kwa mantiki ya kuisoma na kuielewa, bali iliyo na
sura ya kutekelezeka na endelevu kwa ustawi wa taifa la Tanzania. Na ndipo
dhana ya kurekebisha, kuongeza, kupunguza ama kuja na rasimu mpya inapokuwa na
nguvu. Wabunge wakisoma vema wana mamlaka ya kufanya hayo si tu kukaa pale
bungeni na kugonga meza ama kuzomea. Kabla ya kufanya lolote, wabunge wafikirie
dakika watakazozitumia kwa niaba ya watanzania (kama tulivyofafanua hapo juu).
Watanzania wanasubiri
rasimu ya tatu kutoka katika bunge hili. hawatajali kama watakubaliana na hii,
watairekebisha au watatengeneza nyingine, mwsiho wa siku wanasubiri rasimu
watakayoipigia kura ya ama kukubali ama kukataa. kwa waungwana watakubaliana na
mchakato mzima mpaka hapa na wataendelea kusubiri hatua zinazofuata.
Mungu Ibariki
TANZANIA
PAUL C. MAKONDA
Katibu
Wa Hamasa Na Chipukizi UVCCM - 2014
1 Maoni