Unordered List


BAN KI MOON AZINDUA MWONGO WA NISHATI KWA WOTE (2014-2024 )


Na  Mwandishi Maalum, New York 
Katibu  Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban   Ki Moon,  jana alhamisi  amezindua rasmi  mwongo wa Nishati Endelevu kwa wote (SE4ALL)  wakati wa  mkutano  unaohudhuriwa na  wajumbe zaidi wa  1,000 wakiwamo zaidi ya mawaziri 20 wa Nishati 20   wafanyabishara,  mashirika ya kimataifa yakiwamo ya fedha na  Asasi zisizokuwa za kiserikali.

Ujumbe wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu ambao ni  ulioanza  Juni 4 na utamalizika Juni 6, unaongozwa na  Waziri wa  Nishani na Madini Professor   Sospeter Muhongo ( Mb) ambaye  pamoja na  kuhudhuria  na kuchangia mijadala mbalimbali,    ijumaa ( June 6),  atazungumza katika mkutano wa mawaziri kuhusu  nafasi ya Nishati katika  Ajenda  za Maendeleo Endelevu baada  ya 2015.

Akizindua mwongo huo Ban ki Moon, pamoja na mambo mengine alieleza kuwa  licha ya  kuwa pamoja suala la  Nishati ni  suala la kidunia, lakini katika maeneo mengi ni  suala  linalomhusu mwanamke zaidi.


“  Ni suala linalomhusu mwanamke zaidi, linaweza kumaanisha  tofauti kati ya  usalama na hofu, uhuru na  utumwa , hata  uhai na kifo. Dunia  lazima ije pamoja kumaliza  umaskini wa nishati na kuhakikisha watu maskini wanaweza kuhimili maisha yao na kustawi kiuchumi” akasema  Katibu Mkuu.


Akaongeza kuwa  mpango wa  nishati endelevu kwa wote  zimeanza kuzaa matunda na   kwamba ahadi za mabilioni ya dola zilizoahidiwa  zimetolewa.  Huku    nchi zinazoendelea  zaidi ya 80 zimejiunga na  mpango huo.


 Pamoja na  Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kuzungumza wakati wa uzinduzi wa mwongo huo, wengine waliopata nafasi ya kuzungumza ni pamoja na Rais wa Iceland, Olafur Ragnar Grimsson,  Bw. John Ashe,Rais wa Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa na  Rais  wa Banki ya Dunia Jim Yong Kim ( kupitia video) .


Mkutano huu   utafanya  tathmini ya matokeo  ahadi za mabilioni ya dola  kuhusu upatiakani wa nishati, ufanisi wake na nishati mbadala zilizoahidiwa   wafanyabiashara, wawekezaji na watu wengine walizotoa wakati wa Mkutano wa Maendeleo Endelevu ( Rio+20) uliofanyika mwaka 2012.

Aidha  unatarajiwa kuhamasisha    upatikanaji wa raslimali fedha, uwezeshaji  na mipango ya  kufikia  malengo ya  nishati  endelevu kwa wote.

 Waziri wa Nishati na Madini  Profesa Muhongo Sospeter Muhongo (kulia), akiwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  Balozi Tuvako Manongi (kushoti), wakati wa uzinduzi wa Mwongo wa Nishati Endelevu kwa Wote.  Walioketi nyuma ni wasaizidi wa  Waziri.
 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki  Moon, akizungumza wakati wa uzinduzi wa  Mwongo wa Nishati Endelevu kwa  Wote (2014-2024),  uzinduzi huo umefanyika wakati wa Mkutano wa Kwanza wa  Mwaka kuhusu Nishati  Endelevu kwa Wote  ( SE4ALL)unaoendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 1000.  Waziri wa Nishati na Madini,  Mhe. Profesa Sospeter Muhongo ( Mb) anaongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu.

Chapisha Maoni

0 Maoni