TARATIBU ZA KUZINGATIA, KUWA NA WAMILIKI HALALI WA LAINI ZA SIMU
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Mwanadamu
ameumbwa na kuzaliwa akiwa na asili ya kuwa na uwezo na upeo
unaomuwezesha kuwasiliana baina ya mtu na mtu kunzia ngazi ya familia,
jamii inayomzunguka, taifa na hatimaye ulimwengu mzima.
Akiwa na
mamlaka ya kutumia mawasiliano katika maisha yake ya kila siku,
mwanadamu anayatumia mawasiliano hayo kama mchakato wa kuhamisha na
kupashana taarifa ama habari kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa
nyakati tofauti tofauti.
Mchakato
huo wa mawasiliano unaweza kuwa ni mwingiliano unaohusisha ishara kati
ya angalau wakala wawili walio na mkusanyiko wa ishara na sheria za
elimu ishara.
Kwa
mantiki hiyo, mwanadamu anatumia mawasiliano kwa kupasha au
kubadilishana mawazo, maoni, au habari kwa kunena, maandishi, au ishara.
Historia
inasema, mawasiliano yamekuwepo tangu kuwepo mwanadamu hatua inayoleta
mantiki kuwa mawasiliano yamekuwa kongwe kama jamii ilivyo kwani
yamekuwepo tokea enzi za mababu.
Mwanadamu anatumia mawasiliano katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku kulingana na wakati husika.(Martha Magessa)
Ndani ya
mchakato wa kuhabarisha, habari husika hupakiwa, kutumwa na kupashwa na
anayetuma kwa anayepokea kupitia kwa njia maalum kulingana na mahali na
wakati husika.
Mawasiliano
yakishatumwa, anayepokea hupakua ujumbe ule na kumpatia aliyetuma jibu
ama majibu ya alichotaka kujulishwa ambapo mawasiliano yanahitaji
anyetuma ujumbe na anayepokea wapate mrejesho unaoonesha kumekuwa na
mawasiliano sahihi kulingana na mtoa ujumbe.
Ili kuwa
na mawasiliano yenye tija katika jamii, njia zinazohusika na kusikia,
kama vile unenaji, wimbo, na toni ya sauti, na zile zisizohusisha
kusikia, kama vile miondoko ya mwili, lugha ishara, kugusa, kuwasiliana
kwa macho, na kuandika.
Njia hizi
husaidia jamii kupata ujumbe kwa kutumia ishara husika ambazo
zinatarajiwa kuwa ni za kiungwana na zinazojali maadili ya kijamii na
hivyo kuwa na taifa linalojitofautisha na mataifa mengine.
Mawasilano
haya yanaweza kufikishwa kwa kutumia njia ya mdomo ama mazungumzo ya
ana kwa ana, njia ya simu, radio, televisheni, intaneti na mitandao ya
kijamii ambayo imekuwa ni njia ya haraka ya kupashana habari mbalimbali
miongoni mwa jamii.
Kwa kwa
suala la mawasiliano lilivyo nyeti kwa taifa, Serikali imetambua umuhimu
huo na kutoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, wananchi
na umma kwa ujumla kwa kuwatahadhari watumiaji hao wa huduma hiyo
nchini.
Matumizi
mabaya ya mawasiliano na udanganyifu katika usajili wa namba za simu za
mkononi imeonekana kuwa ni tatizo nchini ambapo hivi karibuni Serikali
iliwatahadharisha wananchi kuhusu suala hilo na kuonya kuwa kutumia simu
isiyosajiliwa ama kusajiliwa kwa kutumia taarifa za udanganyifu ni kosa
la jinai.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Meneja mawasiliano wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungy alisema kuwa
kumekuwepo na watu wachache miongoni mwa jamii wanaotumia mawasiliano
pasipo kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa nchini.
Ikizingatiwa
TCRA ni chombo cha Serikali kilichopewa jukumu la kusimamia masuala ya
mawasiiliano nchini, Mamlaka hiyo ilianzishwa kwa sheria. 12 ya mwaka
2003 kusimamia Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta nchini.
Ili
kuendana na wakati, mwaka 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilipitisha Sheria la Mawasiliano ya Elektroniki na Posta (EPOCA)
kusimamia, pamoja na mambo mengine, uuzaji, usajili na matumizi ya laini
za simu za mkononi nchini.
Kwa kuwa
TCRA jukumu lake ni kusimamia mwasiliano nchini, imekuwa mstari wa mbele
mara zote kuwatahadharisha na kuwakumbusha wananchi kwa ujumla
waitambue sheria hiyo ambayo imeainisha makosa yanayotokana na kukiuka
vipengele vya sheria ya mawasiliano.
Miongoni
mwa makosa hayo ni pamoja na kuuza au kusambaza laini ya simu bila
kibali cha mtoa huduma za simu na kuwa na leseni kutoka TCRA na kutumia
laini ya simu ambayo haikusajiliwa.
Makosa
mengine ni kutoandikisha taarifa sahihi za laini husika kabla ya kuitoa
au kuiuza, kutoa taarifa ya uwongo au maelezo yasiyo sahihi wakati wa
kusajili laini ya simu na kuchakachua simu ya mkononi au laini ya simu.
Mnamo Mei
30, 2013 Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Prof. John
Nkoma kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliwataka watumiaji wa
simu za mkononi na wananchi kwa ujumla wa waunge mkono juhudi
zinazofanywa na Serikali ili kufanikisha usajili wa namba za simu kwa
ajili ya kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha
maendeleo ya sekta ya mawasiliano na ya Taifa kwa ujumla.
Zoezi la
kusajili laini za simu, lilikuwa na nia jema ambalo lilimtaka mteja
mtarajiwa kusajili laini ya simu kwa kutoa taarifa sahihi kwa kuonesha
mojawapo ya vitambulisho halisi vyenye picha yake ikiwemo hati ya
kusafiria (Passport), kitambulisho cha kazi, leseni ya udereva, kadi ya
usajili wa mpiga kura, barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mitaa
ikiwa na picha, kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha SACCOs au kadi
ya benki yenye picha ya mhusika halisi anayetaka kusajili laini ya simu.
Haya yote
Serikali imeyaweka ili kuzingatia na kuhakikisha kunakuwa na wamiliki
halali wa laini za simu ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwa jamii.
Kwa kuwa
binadamu ni mrahisi kuelewa na ni rahisi pia kusahau, Serikali imweweka
sheria ambayo iawakumbusha watumiaji wote wa mawasiliano kuwa yeyote
atayekiuka Sheria hiyo ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA)
ya mwaka 2010, kifungu cha 131, sheria hiyo imeainisha kuwa ni kosa la
jinai kutumia au kuwezesha kutumika namba ya simu isiyosajiliwa
kihalali.
Kutokana
na kosa hilo, atakayebainika anatumia laini ambayo haijasajiliwa
atakumbana na adhabu ya faini ya shilingi 500,000 au kifungo cha miezi
mitatu ambayo itatolewa kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo.
Tahadhari
zote hiyo inalenga na kuwashauri watumiaji wa simu za mkononi na
wananchi kwa ujumla wawe tayari kuunga mkono juhudi zinazofanywa na
Serikali ili kufanikisha usajili wa namba za simu kwa ajili ya kudumisha
na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha maendeleo ya sekta ya
mawasiliano na ya Taifa kwa ujumla.
Ni jukumu la letu sote kama wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya mawasiliano kwa maslahi mapana yenye tija kwa umma na Taifa.
Aidha,
Katika vikao vya pamoja na wadau wa mawasiliano nchini vilivyofanyika
Aprili 04 na Aprili 11, 2013, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania na makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi walikubaliana
juu ya hatua za kumaliza kabisa tatizo la usajili wa namba za simu na
utaratibu wa kufungia namba zote za simu ambazo hazikusajiliwa.
Vikao
hivyo vyote viliwahusisha TCRA kwa upande wa Serikali, Watendaji Wakuu
na wawakilishi wa mitandao ya Airtel, BOL, MIC (TIGO), Sasatel, TTCL,
Vodacom na Zantel nchini.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 130 cha sheria ya Mawasiliano ya Elektroniki na
Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, sheria haijambana mtumiaji wa huduma tu,
kwa upande mwingine imewataka wauzaji au wanaotoa kwa namna yoyote ile
namba za simu bila kuzisajili ambapo akibainika atakuwa ametenda kosa la
jinai.
Sheria
imeainisha kuwa adhabu ya kutenda kosa hilo ni kulipa faini ya shilingi
3,000,000 au kifungo cha miezi 12 au adhabu zote zinaweza kutekelezwa
kwa pamoja.
Ili
kuhakikisha mawasiliano nchini yamekuwa yenye tija na yamekuwa kichocheo
cha maendeleo, Serikali iliona kuna haja na sababu za msingi za
kuanzisha utaratibu wa kusajili namba za simu na kupata taarifa sahihi
za watumiaji wake.
Lengo
mahususi likiwa kuwalinda watumiaji na jamii kutokana na matumizi mabaya
ya huduma za mawasiliano, kuimarisha usalama wa taifa pamoja na
kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kuwafahamu vizuri wateja wao na
kuwahudumia ipasavyo kadiri ya mahitaji yao.
Zaidi ya
hapo, Serikali pamoja na makampuni yanayotoa huduma ya mawasiliano
waliona ni vema kuwezesha kuwatambua watumiaji wa huduma za ziada za
simu, kama huduma za kibenki, kutuma na kupokea fedha, kufanya malipo
mbalimbali kwa kutumia simu kwa mfano kulipia huduma za maji, umeme na
vipindi vya televisheni vya kulipia.
Licha ya
mawasiliano kuwa na mabadiliko kadiri ambavyo wakati umepita, teknolojia
imeendelea kukua na kuibua aina mpya na mawazo kuhusu mawasiliano.
Maendeleo
haya ya kiteknolojia yalibadilisha jinsi mawasiliano yanavyofanyika
ambapo watafiti wamegawanya mawasiliano jinsi yalivyobadilika katika
hatua tatu.
Mabadiliko ya mwanzo katika Mawasiliano yalibainisha kuwa maandishi na michoro ndiyo yalianza kutumika kuwasiliana.
Maandishi
hayo yaliandikwa kwenye mawe, ambayo yalikuwa mazito mno kuhamishwa.
Wakati huo, mawasiliano katika maandishi hayangeweza kubebwa, ingawa
yalikuwepo.
Mabadiliko ya pili katika Mawasilianoyalihusisha maandishi ambayo yalianza kutumiwa kwenye karatasi, mavunjo, udongo na nta.
Herufi za
alfabeti zilibuniwa, hivyo kuruhusu mfanano wa lugha katika maeneo
makubwa, ilikuwa ni hatua kubwa baada ya muda, Mjerumani Johannes
Gutenberg aliyeishi kati ya miaka ya 1398-1468, mwaka 1439 alikuwa mtu
wa kwanza duniani kutumia mashine ya kuchapisha magazeti chini ya
shirika aliloliita Gutenberg lililojihusisha na uchapishaji ili
kurahisisha mawasiliano.
Ili
kuhabarisha watu, shirika la Gutenberg lilitayarisha kitabu cha kwanza
cha kuchapishwa kwa kutumia mashine yake ambapo maandiko haya yaliweza
kusafirishwa kwa watu wengine duniani ili wayaone ambayo sasa
mawasiliano hayo ya maandishi yanaweza kuhifadhiwa na kubebwa ikiwemo
magazeti na vitabu.
Mabadiliko
ya tatu ya Mawasiliano yalihusisha taarifa ambayo inaweza kuhamishwa
kupitia mawimbi na ishara za kielektroniki ambayo duniani ndio hatua ya
juu iliyopo ambapo mwanadamu anajivuni mabadiliko ya sayansi na
teknolojia.
Kwa kuwa
Tanzania ni miongoni mwa mataifa ya dunia ya leo imefikia kiwango cha
watu wake kuweza kupata taarifa na kuhamishwa kupitia mawimbi, na ishara
za kielektroniki zilizofikiwa kisayansi duniani, Serikali imeona ni
vema iendelee kutoa tahadhari kwa watu wake ili wawe salama wakati wote.
Yanapotokea
mafanikio katika jamii, wapo wanaotokea kuhujumu mafanikio hayo ndio
maana Serikali kwa kuwajali watu wake imewasisitiza wananchi kujihadhari
na utapeli unaoweza kufanywa kupitia simu za mkononi na mtandao wa
intaneti.
Tahadhari
hiyo iliyotolewa na Serikali inasisitiza kutokutekeleza maagizo yoyote
yanayohusu fedha kwa ujumbe wa maandishi hata kama yanatoka kwa mtu
unayemfahamu, mmliki wa simu kutumia namba ya siri ambayo sio rahisi mtu
mwingine kukisia na kutokutoa namba za siri za anazotumia mmiliki wa
simu katika masuala yanqayohusu miamala ya kifedha.
Tahadhari
nyingine ni kutokutekeleza maagizo yoyote kutokana na ujumbe wa simu za
mkononi unaomtaka mtumiaji wa simu kutuma fedha kutoka namba ambayo
mtumiaji wake unamfahamu na ambao unakueleza kuwa simu yake inahitilafu,
hivyo hawezi kuongea, usitekeleze maagizo hayo.
Zaidi ya
hayo, mtumiaji wa simu anatakiwa kutumia namba ya siri ambayo sio rahisi
mtu mwingine kuikisia, kutokutoa namba za siri anazotumia mteja wa simu
na kuhakikisha namba ya mtu unayemtumia pesa au salio kabala ya kutuma.
Aidha,
mmliki wa simu akipoteza simu yake au laini anapaswa kutoa taarifa kwa
mtoa huduma aliyeko karibu nae na aende polisi mara moja kutoa taarifa
hiyo.
Endapo
mteja asipopata ushirikianaoa wa kutosha kwa mtoa huduma aliyeko karibu
yake, mteja anapaswa kuwasilisha malalamiko hayo kwa TCRA.
Njia
sahihi za kufikisha malalamiko ni pamoja na kuyatuma kwa kuandika
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, S. L. P. 474 Dar es salaam ama kufika
ofisi za TCRA makao makuu Dar es salaam au ofisi za kanda na Zanzibar.
Namana nyingine ni kupiga simu namba 0784558270 au 0784558271 na kwa barua pepe malalamiko@tcra.go.tz aucomplaints@tcra.go.tz .
Pamoja na
baadhi ya tahadhari hizo, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri
kwenye Sekta ya Mawasiliano ambayo yameonesha inaendelea kukua nchini na
imekuwa na matokeo makubwa.
Kadiri siku zinavyokwenda, kumekuwa na idadi ya kubwa ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Idadi
hiyo imeendelea kuongezeka kutoka laini za simu za kiganjani milioni
2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 27.45 mwezi Desemba 2013 ambapo
watumiaji wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka milioni 3.56
mwaka 2008 hadi kufikia milioni 9.3 mwezi Desemba 2013.
Vilevile,
mawasiliano nchini yanavyozidi kuongezeka, kumekuwa na ongezeko kubwa
la huduma kupitia mawasiliano ya simu za kiganjani ambapo huduma za
kifedha zinazotolewa kwa watumiaji wa simu hizo zimeongezeka pia.
Katika
kudhihirisha hilo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof.
Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), katika hotuba yake wakati akiwasilisha
Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2014/2015
mwezi Mei mwaka huu alisema kuwa huduma zilizoongezeka ni pamoja na
miamala ya kifedha ambayo ina watumiaji wapatao 12,330,962 na ununuzi wa
huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki.
"Hivi
sasa, wananchi wanaweza kufanya malipo ya huduma mbalimbali
wanazozitumia kupitia simu za kiganjani" alisema Prof. Mbarawa.
"Katika
kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014 kuna jumla ya miamala 972,
641,605 yenye thamani inayofikia shilingi Trilioni 28.3 imefanyika",
aliongeza Prof. Mbarawa.
Prof.
Mbarawa alisisitiza kuwa maendeleo hayo yamesaidia kuokoa muda wa
wananchi na kupunguza msongamano sehemu za kulipia na kupata huduma hizo
wanazohitaji kwa wakati bila usumbufu wowote.
Maendeleo
hayo ndiyo yanayoisukuma Serikali kupitia TCRA kujiwekea malengo katika
mwaka wa fedha 2014/2015 ambayo itatekeleza kwa kufanya tathmini ya
gharama za huduma za simu za mkononi na kufanya utafiti kuhusu utoaji wa
huduma za intaneti na matumizi ya masafa yanayowezesha mawasiliano ya
intaneti (Broadband) ili yaboreshwe na kufikia wanachi wengi zaidi na
kupata mawasiliano yenye tija manufaakwa taifa.
Aidha,
alipokuwa akihitimisha hotuba yake, Prof. Mbarawa aliyashukuru makampuni
ya simu za kiganjani kwa kuwa tayari katika kushughulikia changamoto za
mawasiliano katika maeneo yasiyo na mawasiliano hapa nchini.
Mbali na
huduma ya mawasiliano, Prof. Mbarawa alisema kuwa makampuni hayo ya simu
nchini yamekuwa tayari katika kuchangia maendeleo na upatikanaji wa
huduma za jamii zenye tija kwa wananchi.
Makampuni
hayo yameonesha nia ya dhati na kushiriki katika shughuli mbalimbali za
kijamii kama vile uchangiaji wa damu salama, ujenzi wa vituo vya afya,
ununuzi wa vitabu vya ziada na kiada vinavyotumika mashuleni na vyuoni,
ununuzi wa madawati na ujenzi wa madarasa.
Tukiwa
kwenye ulimwengu wa utandawazi, kama nchi ni vema kusimamia maadili ya
Kitanzania na utamaduni wetu mwema unayoipambanua nchi yetu na mataifa
mengine kwa kuzingatia misingi ya utaifa wetu.
Tuyatumia mawasiliano kama sekta muhimu nchini ili taifa lifikie malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Maenedleo
hayo hayawezi kufikiwa kama Watanzania wote kwa umoja wao, nchi na
mashirika ambayo ni washirika wa maendeleo, watatumia vibaya mwasiliano
kwa lengo la kubomoa badala ya kujenga.
Hima hima
TCRA, jukumu mlilopewa na taifa la kusimamia mawasiliano ni nyeti,
juhudi zenu zisonge mbele ili watumiaji visivyo wa mawsiliano
wachukuliwe kuwa ni wahujumu maendeleo ya taifa letu.
Ni suala
la kiungwana na la kisheria kwa watumiaji wa simu za kiganjani kusajili
namba zao za simu mbapo TCRA mara zote inawahimiza kusajili laini zao za
simu.
Ili
kujihakikishia kuwa laini yako ya simu imesajiliwa ni vema mtumiaji wa
simu husika kuthibitisha na kijiridhisha kama usajili wake upo sahihi
kwa kupiga *106# kwenye simu yako.
Uhakiki
huo unahusisha watumiaji wa huduma ya mawasiliano kupitia mfumo wa
makampuni ya Vodacom, Airtel, Tigo na Zantel, SASATEL na TTCL Mobile, na
watasikiliza maelekezo.
Taarifa
utakayoipata inatakiwa kutaja jina lako kama mtumiaji halali wa namba
husika, na iwapo utapata jibu tofauti, tafadhali fika kwenye ofisi ya
mtoa huduma wako au wakala wake ili kurekebisha kasoro hizo.
Watumiaji
wa simu za mkononi na wananchi wanashauriwa kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na Serikali ili kufanikisha usajili wa namba za simu kwa
ajili ya kudumisha na kuendeleza amani na usalama na kuharakisha
maendeleo ya sekta na ya Taifa kwa ujumla.
0 Maoni