Unordered List


TANZANIA YAZIDI KUSONGA

TANZANIA YAJIVUNIA KUFIKIA MALENGO YA MILENIA KATIKA AFYA, ELIMU


DSC_0564
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya Umoja wa Mataifa inayotarajiwa kuanza kuadhimishwa Ijumaa wiki hii (kushoto) ni Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.
Na Mwandishi Wetu
KATIBU MKUU wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule amesema serikali ya Tanzania imefikia kwa kiwango kikubwa baadhi ya malengo ya milenia ya afya na elimu. MOblog Tanzania inaripoti
Akizungumza katika mahojiano maalumu na MOblog Tanzania ofisini kwake jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza mkutano na wanahabari juu ya wiki ya Umoja wa Mataifa inayotarajiwa kuanza Ijumaa wiki hii, Haule amesema Tanzania imeyafikia kwa kiwango kikubwa malengo ya milenia katika afya na elimu.
“Serikali ya awamu nne kwa kiwango kikubwa imefikia baadhi ya malengo ya milenia hasa katika elimu na afya kwa kujenga shule za msingi na sekondari katika kila kata na vituo vya afya nchi nzima,” amesema Haule.
Amesema kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa katika kufikia maendeleo katika kila nyanja duniani.
Aliongeza kwamba ni muhimu nchi zote duniani kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanapatikana kwa pamoja na hakuna nchi inayoachwa nyuma.
Haule alisisitiza kwamba katika kuadhimisha wiki ya Umoja wa Mataifa serikali itaendelea kutoa ufafanuzi kwa wananchi umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika kila jambo linalofanya na Umoja wa Mataifa.
“Umoja wa Mataifa unatimiza miaka 69 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945 mafanikio mengi yamepatikana na changamoto bado zipo nyingi lakini nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa wataendelea kushirikiana na umoja huu kutimiza lengo kuu la maendeleo dunia nzima,” alifafanua
DSC_0574
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, John Haule akiteta jambo na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.
Amesema kwamba katika mpango mkakati wa Umoja wa Mataifa juu ya malengo mapya ya kuanzia mwaka 2015-2030 serikali imejipanga kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.
Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, amesema kwamba Umoja wa Mataifa itaendelea kushirikiana na nchi zote wanachama ikiwemo Tanzania katika harakati za kuondoa umaskini.
“Malengo ya milennia yamefanya nchi nyingi wanachama kufanya kazi kwa bidii katika kupunguza umaskini wa kipato, fursa ya elimu na upatikanaji wa matibabu kwa njia nafuu kwa maelfu ya watu duniani,”
Aliongeza kwamba katika kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa ya kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii inalenga kuwakutanisha pamoja nchi zote katika kila hatua ya maendeleo dunia nzima.
Rodriguez amesema kwamba Umoja wa Mataifa na malengo yake ni kuhakikisha usawa wa kiuchumi na kijamii unafikiwa katika jamii pana iliyo huru kwa kumshirikisha kila mtu katika maamuzi ya maendeleo.

Chapisha Maoni

0 Maoni