Unordered List


MKUTANO WA CCM WA MABALOZI WILAYA YA AMANI MKOA WA MJINI

unnamedRais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akipokea Taarifa ya Chama Wilaya Amani kutoka kwa Katibu Abdalla Mwinyi katika mkutano wa Mabalozi wa Mkoa wa Mjini  Unguja akiwa katika ziara yake ya kuimarisha Chama cha Mapinduzi katika Mikoa ya Unguja,[Picha na Ikulu.]

unnamed1Mwenyekiti wa CCM MKoa wa Mjini Mhe,Borafya Silima Juma akiwapa nasaha Mabalozi wa CCM Mkoa wa Mjini katika wilaya ya Amani wakati mkutano wa kuimarisha Chama cha Mapinduzi ikiwa ni mfululizo wa ziara ya Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein,[Picha na Ikulu.]
unnamed2Mumbewa Mkutano wa Mabalozi wa Wilaya ya Amani CCM kutoka Mpendae Gabriel Mlekwa akitoa mchango wake katika mkutano maalum wa Mabalozi wa Wilaya hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa  Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akiwa katika mfululizo wa ziara ya kuimarisha Chama katika Mkoa wa Mjini Unguja,[Picha na Ikulu.]
unnamed4Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Mabalozi wa Majimbo mbali mbali ya  wilaya ya Amani Unguja akiwa katika mfululizo wa ziara zake za kuimarisha Chama katika Mkoa wa Mjini Unguja katika ukumbi wa CCM Mkoa Amani leo,[Picha na Ikulu.]
………………………………………………………………………………………………..
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakishia wananchi kuwa Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa matatizo mbalimbali yanayowakabili yanapatiwa ufumbuzi kwa wakati kulingana na mipango na uwezo wa serikali.
“hatushabikii maovu wala matatizo ya wananchi. Serikali kwa ujumla wake inachukua hatua mbalimbali na kupanga mipango madhubuti kuona matatizo hayo yanapatiwa ufumbuzi” Dk. Shein alisisitiza.
Akizungumza na mabalozi wa nyumba kumi na viongozi wa Maskani za Chama cha Mapinduzi wilaya ya kichama ya Amani mjini Unguja leo, Dk. Shein amesema ni bahati mbaya kuona kuwa wakati mwingine baadhi ya wanasiasa wanajaribu kuyaeleza matatizo hayo kuwa ni mambo madogo yanayoweza kuondolewa mara moja.
“Kwa mfano suala la ajira si jambo dogo kama baadhi ya watu wanavyojaribu kulieleza kwa wananchi ili kujipatia manufaa ya kisiasa. Hii inanitia shaka kwa kiongozi kufanya jambo hilo” Dk. Shein alieleza.
Alifafanua kuwa ajira si tatizo la Zanzibar pekee bali duniani kote na kutoa takwimu zikionesha kuwa tatizo hilo kwa sasa Zanzibar limefikia asilimia 17 ya watu wote na kati ya hao vijana ni asilimia 14.
 “Ningependa kuona vijana wote na wananchi wa Zanzibar wana ajira lakini sisi hatujawa na uwekezaji mkubwa wa kutoa ajira nyingi wala ardhi kubwa ya kukidhi mahitaji ya ajira kwa watu wetu” Dk. Shein aliongeza.
Kwa hivyo aliwaeleza kuwa ndio maana Serikali imeamua kuwahamasisha vijana wanaomaliza masomo yao pamoja na makundi mengine kujiajiri na serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo kuwawezesha ili kumudu kujiajiri.
Tatizo la ajira pamoja na huduma zisizoridhisha katika Hospitali Kuu ya Mnanzi mmoja ni miongoni mwa masuala yaliyogusiwa na viongozi waliopata fursa ya kutoa maoni yao ambapo Mhehimiwa Rais alitumia fursa hiyo kuyatolea ufafanuzi baadhi yake.
Kuhusu huduma katika hospitali hiyo kuu iliyopo mjini Unguja, Dk. Shein aliwahakikishia kuwa taarifa ya baadhi ya mapungufu anazo na anafuatilia kwa karibu suala la uimarishaji wa huduma katika hospitali hiyo na nyingine humu nchini.
Alifafanua kuwa hivi sasa kuna hatua nyingi zinazochukuliwa katika kuimarisha hospitali hiyo kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo na hatua hizo ni katika kutekeleza azma ya serikali kuimarisha huduma za rufaa katika hospitali hiyo.
Kuhusu utelekezaji wa agizo lake la kutaka wajawazito wasitozwe fedha wakati wa kujifungua iwe kwa njia ya kawaida au kwa upasuaji, Dk. Shein alisema lipo tatizo la kutotekelezwa kikamilifu agizo hilo lakini alifafanua kuwa hali hiyo wakati mwingine inatokana na wizara ya Afya kutopata fedha za matumizi mapema lakini pia wakati mwingine ni matatizo ya baadhi ya watumishi wa afya.
Kwa hivyo aliwaahidi kuendelea kufuatilia suala hilo na mengine ambayo viongozi hao walimueleza wakati wa kutoa maoni yao.
“Serikali yenu ni sikivu, lazima tuzingatia maoni yenu na hoja zenu kwani ni za msingi hivyo tunahitaji kuzitafakari na kuzifanyia kazi kwa kuwa tunapaswa kuzijibu kwa umakini ” Dk. Shein aliwaambia viongozi hao.
Katika mkutano huo, Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, aliwataka wana CCM kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupambana na maovu katika jamii  ikiwemo vitendo vya udhalilishaji wa watoto na wanawake na kwamba yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele kuvikemea vitendo hivyo kila anapopata fursa ya kufanya hivyo.
Mapema Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo ya kichama ya Amani Abdi Ali Mzee mbali ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kusimammia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa lakini pia alitoa wito kwa Mawaziri kwenda kwa wananchi kuwaeleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana na katika kutekeleza mipango ya maendeleo.
“Tunaomba shughuli za utekelezaji wa Ilani zitangazwe na kuoneshwa katika televisheni na vyombo vingine vya habari ili wananchi waweze kuelewa ili kuepuka upotoshaji ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu” alisema Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliwaambia viongozi hao kuwa Katiba iliyopendekwa si ya Chama cha Mapinduzi kama baadhi ya watu wanavyoeleza bali ni ya wananchi wote wa Zanzibar kwani wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliopitisha kwa theluthi mbili kutoka Zanzibar wametoka katika makundi yote.
“Tuwapongeze wabunge hao kwa ujasiri wao na kutetea maslahi ya Zanzibar katika Katiba iliyopendekezwa ” alisema Bwana Vuai.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Chapisha Maoni

0 Maoni