Unordered List


PINDA AONGEZA NGUVU KUPAMBANA NA UJANGILI



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (wapili kushoto) na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey Mwanri (kulia) baada ya kufunga Mkutano wa kupiga vita ujangili wa wanayamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanayamapori mjini Arusha Novemba 8, 2014. Kushoto ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli.Wapili kulia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dkt Richard Sezibara(Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
........................................................................................
* Ataka iundwe timu kufuatilia utekelezaji wa Azimio la Arusha 2014
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema inahitajika dhamira ya kweli kutoka kwa wadau wote katika kutekeleza Azimio la Arusha la kukabiliana na ujangili na kuendeleza hifadhi za wanyama katika nchi za Afrika Mashariki na zilizo Kusini mwa Ikweta.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni (Jumamosi, Novemba 8, 2014) mara baada ya kufunga mkutano wa kikanda wa siku mbili uliojadili mbinu za kupambana na biashara haramu ya wanyamapori ulioandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha, Waziri Mkuu alisema: "Suala hili linataka uwajibikaji wa pamoja. Mashirika na taasisi, wananchi na viongozi sote kama wadau wakuu, kila mmoja anapaswa kushiriki vita hii kama kweli tunataka tuitokomeze."
"Kwenye hili Azimio la Arusha na nyie waaandishi wa habari pia mna sehemu yenu mmetajwa... wamesema wanatafuta jinsi ya kushirikiana na vyombo vya habari ili visaidie kutoa elimu kwa jamii kama njia ya kuelimisha umma," alisema.
Waziri Mkuu aliwaeleza waandishi hao kwamba Azimio hilo lina vipengele 20 ambavyo vinataka utekelezaji katika ngazi ya nchi mojamoja, ngazi na kanda na ngazi ya kimataifa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
"Nimepata faraja kwamba mkutano huu haukuisha kijumlajumla tu, bali umekuja na maazimio 20 ambayo yametengwa kwa ajili yetu sisi wa ndani, mengine yanahusisha ushirikiano wa kikanda na yako mengine yanawahusisha wadau wa maendeleo," alifafanua.
Ili kutekeleza azimio hili, nimeshauri iundwe timu itakayoshirikisha vyombo vingi zaidi badala ya kuiachia Wizara ya Maliasili na Utalii peke yake. Timu hii ikutane kila baada ya miezi sita ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya na ikibidi Waziri atoe taarifa bungeni kuhusu utekelezaji huo," alisema Waziri Mkuu.
Mapema, akizungumza na washiriki wa mkutano huo wakati wa kuufunga, Waziri Mkuu alisema kuwepo kwa watu wa ngazi tofauti kwenye mkutano huo ni kielelezo tosha cha umakini wao na nia thabiti ya kutokomeza ujangili katika ukanda huu.
"Tumeanzisha vita, tusisahau kwamba bado kuna kazi kubwa mbele yetu na vita haijaisha. Tuzidishe mapambano katika sehemu tatu: kwenye nchi unakofanyika ujangili, nchi ambazo nyara zinapitishwa na nchi zinazopokea ama kununua hizo nyara," alisema Waziri Mkuu.
"Nakubaliana nanyi kwamba hakuna nchi inayoweza kukabili suala la ujangili ikiwa peke yake. Tunahitaji tuwe na sera mahsusi, sera ya pamoja ya kutuunganisha na kutuongoza wakati tukitekeleza Azimio hili kwa kusaidiana na wadau wa maendeleo," alisema.
Alisema Azimio hilo litaipa kazi ya ziada ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo kazi kubwa itakuwa ni kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa wa Azimio hilo unakuwa wa ufanisi.
Jumla ya nchi tisa zimetia saini azimio hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo ni Burundi, Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia, Rwanda na Malawi.CHANZO FULL SHANGWE

Chapisha Maoni

0 Maoni