Unordered List


TARATIBU ZA TIBA YA RAIS MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE ZAKAMILIKA

D92A4106
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akitoka katika hospitali ya Johns
Hopkins iliyopo Baltimore Maryland baada ya kutolewa nyuzi katika
mshono baada ya kufanyiwa upasuaji wiki iliyopita.
………………………………………………………………….
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI LEO
Taratibu za matibabu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, zimekamilika leo, Jumatatu, Novemba 24, 2014.
Taratibu hizo za matibabu za Mheshimiwa Rais Kikwete zimekamilika kiasi cha saa 12 asubuhi ya leo wakati madaktari bingwa katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko mjini Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, walipomfanyia hatua ya mwisho ya tiba.
Hata hivyo, Rais Kikwete ataendelea kupumzika na kuangaliwa kwenye Hoteli Maalum inayohusiana na Hospitali ya Johns Hopkins kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani.
Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa na madaktari, Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani Jumamosi, Novemba 29, 2014.
Rais Kikwete aliondoka nchini Alhamisi ya Novemba 6, 2014, kwenda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake lakini madaktari katika Hospitali ya Johns Hopkins waliamua kumfanyia upasuaji wa tezi dume Jumamosi ya Novemba 8, 2014.
Rais Kikwete anaendelea kuwashukuru Watanzania kwa sala na maombi yao ya kumtakia heri ya kupona haraka na kurejesha afya njema katika kipindi chote cha ugonjwa wake.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Novemba,2014

Chapisha Maoni

0 Maoni