Unordered List


MAMA KIKWETE AWATAKA VIJANA KUJIUNGA NA VIKUNDI VYA KUWEKA AKIBA NA KUKOPA ILI KUKABILIANA NA TATIZO LA AJIRA

unnamed
Na Anna Nkinda – Maelezo
18/12/2014 Vijana wametakiwa kujiunga na vikundi vya kuweka akiba na kukopa  ili kuchangia mawazo yao  na ubunifu na wakati huo huo wanajitengenezea mazingira ya kujiajiri kwani wengi wao wana elimu na ujuzi walioupata  masomoni lakini wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira.
Rai hiyo imetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizindua Umoja wa Vikundi vya kuweka Akiba vilivyopo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) wilaya ya Kinondoni (UWAMAKI) katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Usafirishaji jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema kupitia vikundi hivyo vijana wanaweza kupata mitaji midogomidogo pamoja na mafunzo ya kuwawezesha kuanzisha biashara na kujiajiri. Kwani mfumo huo wa vikundi na mafunzo ni moja ya njia za kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na hivyo kupunguza tatizo la ajira.
Kwa upande wa wanachama wa UWAMAKI aliwasisitiza  kutoridhika na mafanikio waliyoyapata bali waendelee kutafuta njia za kupiga hatua hususani kupata utaalamu wa kuboresha bidhaa zao , kutafuta masoko zaidi na kufanya ubunifu wa kuweza kuvumbua bidhaa na biashara nyingine tofauti ili kuepukana na ushindani wa soko.

“Mnapokuwa na bidhaa zinazofanana mtakuwa katika mazingira ya kushindania soko jambo ambalo litapunguza kiasi cha mauzo ambayo ndiyo pato lenu wajasiriamali. Jitihada ifanywe ili kuweza kutafuta watalaam ambao watawapa mafunzo ya kukuza biashara”, alisema Mama Kikwete.
Akisoma risala ya vikundi hivyo Katibu wa UWAMAKI , Mwajuma Waziri aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuwawezesha  kuwa na vikundi na kupata mafunzo ya kuweka akiba, elimu ya kibenki, usindikaji wa vyakula na huduma ya bima ya afya.
Waziri alisema, “Kutokana na mafunzo hayo tunaweza kuanzisha miradi mbalimbali kama vile kutengeneza sabuni za maji za kufulia, sabuni za kuoshea vyombo na kusafishia tairizi, siagi ya karanga na batiki na hatimaye tumeweza kufungua akaunti yetu ya Umoja katika benki ya wanawake (TWB)”.
Katibu huyo alisema walianza na kikundi kimoja kwa kujiwekea hisa moja kwa thamani ya shilingi 1000 pia waliweza kukopesha kiasi cha shilingi 6,300,000 mpaka mwisho wa mwaka walivuna shilingi 12,750,000.
“Hadi sasa tunavikundi 11 vyenye wanachama 274 kati ya hao wanaume ni wanane katika vikundi hivi  tumeweza kukopesha kiasi cha shilingi 47,500,000/= na kufikia mavuno ya shilingi 79,739,000 kwa mwaka”, alisema.
Alimalizia kwa kusema lengo la kuunda umoja huo ni kushirikiana katika matatizo ya kijamii, kuunda SACCOS na kutafuta masoko ya bidhaa zao.
Taasisi ya WAMA inasimamia mradi wa kuwawezesha wanawake kwa kuwapa mafunzo kupitia vikundi katika mikoa ya Dar es Salaam Lindi na  Pwani hadi kufikia Septemba mwaka huu jumla ya watu 18,000 wamefikiwa kwa kupitia vikundi 688 vilivyoundwa na tayari shilingi milioni 227 zimekusanywa na kukopeshwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni