Unordered List


TAARIFA YA UFAFANUZI WIZARA YA NISHATI NA MADINI

Katika gazeti la NIPASHE la Jumatatu tarehe 08 Desemba, 2014 ziliandikwa habari kuhusu Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb) chini ya kichwa cha habari “Wanaomtetea Muhongo Wajibu haya”. Hoja zilizotolewa katika gazeti hilo zililenga kupotosha ukweli. Wizara inapenda kutoa maelezo kuhusu hoja zilizotolewa kama ifuatavyo:
Utendaji wa Wizara chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb)
Taarifa za gazeti hilo zilieleza kuwa utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini hasa katika uongozi wa Waziri Muhongo umekuwa ni wa kukatisha tamaa. Moja ya mifano iliyotolewa ni kuendelea kuwepo kwa wachimbaji madini wanaozidi kutorosha madini kwa nia ya kukwepa kodi. Hoja hii haina ukweli wowote kwani chini ya uongozi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb) utendaji wa Wizara umeimarika kwa kiasi kikubwa. Chini ya Uongozi wake kumekuwepo na uwajibikaji mkubwa kwa watumishi wa wizara ili kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi ipasavyo. Ni katika kipindi chake kumekuwepo na uanzishwaji wa madawati ya ukaguzi wa madini katika viwanja vikubwa vya ndege vya JNIA, KIA na Mwanza chini ya Wakala wa Ukaguzi wa madini (TMAA) ili kudhiditi wachimbaji madini na watu wengine wenye nia ya kutorosha madini nje ya nchi bila kuzingatia sheria. Kutokana na hatua hiyo madini mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15 yameweza kukamatwa. Madini yaliyokatwa bila kuwa na vibali halali
yametaifishwa na Serikali. Serikali ilianza kuuza baadhi ya madini yaliyokamatwa kwa njia ya mnada kwenye Maonyesho ya Vito yaliyofanyika Mjini Arusha kuanzia tarehe 18 – 20 Novemba, 2014. Katika mnada huo jumla ya zaidi ya shilingi milioni 70 zilipatikana na kuingia Serikalini. Serikali itaendelea kupiga mnada madini mengine yaliyokamatwa kwa manufaa ya taifa. Wizara inaendelea kuimarisha udhibiti ili kuhakikisha kuwa mtu yeyote anayekusudia kutorosha madini anakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na madini yake kutaifishwa na Serikali. Katika kusimamia sheria na taratibu, chini ya Uongozi wa Prof.Muhongo, Wizara imedhibiti tabia ya kuchukua vitalu vya madini na kuhodhi ili wale tu wanaozingatia masharti ya leseni ndio waendelee kuvifanyia kazi vitalu. Hili limewaumiza waliokuwa na tabia hiyo ambao kimsingi walikuwa wanavunja sheria. Baadhi ya vitalu vilivyopokonywa vimekuwa vikigawiwa kwa wachimbaji wadogo.Hivyo, si kweli kwamba utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini chini ya Prof. Sospeter Muhongo (Mb) ni wa kukatisha tamaa katika kudhibiti utoroshaji wa madini nje ya nchi na katika ukiukwaji wa masharti ya leseni mbalimbali za madini kama ilivyodaiwa.
Upitiaji Mikataba ya Madini
Taarifa za gazeti hilo la NIPASHE la Jumatatu tarehe 08 Desemba, 2014 zilieleza kuwa chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb) Serikali imeshindwa kupitia mikataba ya madini ili taifa linufaike zaidi. Taarifa hizo si za kweli zinalenga kupotosha umma.
Ukweli ni kuwa chini ya Uongozi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (Mb), Wizara imepitia mikataba ya madini kwa kufanya majadiliano na Kampuni za uchimbaji madini zenye mikataba ili kurekebisha vipengele vya mikataba ambavyo vinalenga kuleta manufaa zaidi kwa Taifa. Kazi hiyo imefanyika kwa Kampuni zote zenye mikataba na tarehe 9 Oktoba, 2014 Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) imetiliana saini mkataba wa kurekebisha vipengele katika mkataba uliosainiwa huko nyuma baada ya majadiliano kukamilika. Aidha, majadiliano na Kampuni ya ACACIA (zamani Kampuni ya African Barrick Gold –ABG) yamekamilika na kilichobaki ni pande mbili (Serikali na Kampuni) kusaini marekebisho yaliyofanyika kwa ajili ya mikataba ya migodi yake ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.
  1. KUKATIKA KWA UMEME
Kukatika kwa umeme kunasababishwa na kuzeeka kwa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme. Ikumbukwe kuwa, kwa kipindi cha karibu miaka kumi TANESCO iliwekwa chini ya PSRC kwa nia ya kubinafsishwa mwaka 1997 – 2007. Katika kipindi hiki TANESCO haikuruhusiwa kuwekeza wala kufanya ukarabati wa miundombinu yake hivyo hali hiyo ilipelekea kuchakaa kwa miundombinu hiyo ikiwemo mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme. Hata hivyo baada ya Serikali kubadili mtazamo wake wa kulibinafsisha Shirika, TANESCO mipango kabambe ya kufanya ukarabati wa miundombinu hiyo na kujenga mipya ili kuwa na mfumo wa usafirishaji na usambazaji umeme ulio wa uhakika. Kazi hiyo inaendelea katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo jiji la Dar es Salaam ambako kazi ya kukarabati na kupanua miundombinu ya usambazaji umeme inaendelea. Aidha, TANESCO ilishaelekezwa kutoa taarifa kwa umma kuhusu katizo lolote la umeme lililopangwa kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya umeme. TANESCO imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vyombo vya habari vikiwemo televisheni, radio na magazeti na pia kwa kutumia magari ya TANESCO kufikisha taarifa kwa maeneo yanayoathirika. Kwa upande wa katizo la umeme usiotarajiwa, TANESCO inacho kikosi cha dharura ambacho watumishi wake wanafanya kazi masaa ishirini na nne kwa zamu ili kuhakikisha kuwa hitilafu ndogondogo zinatatuliwa mara moja zinapojitokeza. Jamii ya Watanzania wanalishuhudia hilo.
  1. DENI LA TANESCO LAPAA.
Mpaka kufikia mwanzoni mwa mwaka 2014, deni la TANESCO lilikuwa limefikia takribani Shilingi bilioni 695.30. TANESCO kwa kutumia vyanzo vyake vya fedha kutokana na ukusunyaji wa maduhuli ndani ya kipindi cha miezi 11 imepunguza deni hilo mpaka kufika takribani Shilingi bilioni 355.11. Kukua kwa deni la TANESCO kulisababishwa na hali ya ukame uliolikumba taifa kuanzia miaka ya 2011 ambapo TANESCO ililazimika kununua umeme aghali kutoka kwa wazalishaji wa umeme binafsi ikiwemo mitambo ya kukodi ya dharura. Deni hilo lilikua kama ifuatavyo:
Mwaka Deni (Bilioni Sh.)
2011           538.47
2012            563.02
2013           695.30
2014 (9 Disemba) 355,11
TANESCO imeongeza ufanisi wake katika kukusanya maduhuri na kufikia kiwango cha asilimia 97 na fedha inayopatikana inatumika kupanua huduma ya umeme nchini, kuendesha Shirika na kulipa madeni inayodaiwa.
Ukweli ni kwamba deni la TANESCO limeshuka kwa kiasi kikubwa na kwa sasa TANESCO imeweka mkakati maalumu wa kuwalipa wadeni wake wakubwa kiasi cha Shilingi bilioni tatu kwa wiki kwa kila mdai, hivyo ni matarajio ya Shirika kumaliza deni hilo mwaka kesho (2015).
  1. NCHI ITASONGA MBELE
Wazo la kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) lilibuniwa na watumishi na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2005/6 chini ya uongozi wa Nazir Karamagi akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Taratibu za kuanzishwa kwa REA zilikamilika mwaka 2007 ambapo REA ilianza kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Sospeter Muhongo baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini ameisaidia REA kupata fedha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na hivyo amesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza kwa kasi ya kupeleka huduma ya umeme vijijini.
Aidha, Ili kufikia lengo la kuwaunganishia umeme asilimia 30 ya watanzania ifikapo mwaka 2015, Chini ya uongozi wa Waziri Muhongo Serikali kupitia TANESCO, ilipunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (single phase) kwa wateja wadogo kwa wastani wa kati ya asilimia 30 na 77 kama ifuatavyo:
  1. Kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) kwenye umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 177,000 na wa mijini watalipa Shilingi 320,960 badala ya Shilingi 455,108 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.

  1. Kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja, katika maeneo ya vijijini ni Shilingi 337,740 na wa mijini ni Shilingi 515,618 badala ya Shilingi 1,351,884 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.

  1. Kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini ni Shilingi 454,654 na wa mijini ni Shilingi 696,670 badala ya Shilingi 2,001,422zinazolipwa na wateja hao kwa sasa.

Kwa ujumla katika kipindi hiki huduma ya umeme nchini imepanuka na kuwa bora zaidi kuliko siku za nyuma. Ni matarajio ya Serikali kuwa huduma hii itazidi kuwa bora zaidi katika siku chache zijazo kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea katika sekta ndogo ya umeme.
  1. DALALI WA FEDHA ZA ESCROW
Waziri wa Nishati na Madini ndiye msimamizi mkuu wa masuala yanayohusu sekta za Nishati na Madini nchini. Mtambo wa IPTL ulijengwa kwa ajili ya kufua umeme unaotumiwa na jamii ya watanzania. Kuwepo kwa mgogoro kungeweza kuondoa azma ya uwepo wa mtambo huo ya kufua umeme ili kuliepusha Taifa kuingia katika mgawo wa umeme kutokana na upungufu wa upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo lilikuwa ni jukumu lake kuona kuwa mgogoro wa wawekezaji wa mitambo ya IPTL unakwisha ili mitambo iendelee kutoa huduma ya umeme kwa Taifa. Jukumu la Waziri ni kusimamia Sera, Sheria na taratibu katika sekta anazozisimamia. Katika kufanya hivyo, Waziri hukutana na wadau na kujadili masuala kwa uwazi bila kificho kwa nia ya kujenga nchi na kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele. Kwa hiyo mikutano na Wadau ikiwa ni pamoja na wawekezaji hufanyika si kwa udalali. Suala la fedha za akaunti ya Escrow lilihusu uamuzi wa mahakama iliyojiridhisha kuwa mnunuzi wa hisa zote za VIP na MECHMAR ni halali na alitakiwa kukabidhiwa mali na madeni ya IPTL. Mali ni pamoja na kiasi cha fedha stahiki kwenye Akaunti ya Escrow ambazo hata hivyo ilidhihirika kuwa hazitoshi kukidhi deni halali.
Akaunti hiyo ilikuwa na Sh. 182 bilioni wakati malipo yaliyokubalika kwa pande zote (IPTL na TANESCO) kwa mujibu wa maamuzi ya ICSID I yalikuwa Sh. 306 bilioni. Kumwita Waziri wa Nishati na Madini kuwa ni dalali ni kupotosha ukweli.

Chapisha Maoni

0 Maoni