Unordered List


REA AWAMU YA PILI KUKAMILIKA JUNI

mzu
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akitoa maelekezo kwa mtaalamu kutoka kampuni ya Symbion iliyopewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika kijiji cha Nyamikoma kilichopo wilayani Busega Bw. Steve Thomson (kushoto)
• Vijiji 1,500 kupatiwa umeme 
Na Greyson Mwase, Busega
Imeelezwa kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu mradi wa usambazaji wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) unatarajiwa kukamilika, ikiwa ni pamoja na kuvipatia umeme vijiji 1,500.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kwa nyakati tofauti alipofanya ziara katika vijiji vya Ihale, Bukombe, Nyamikoma, Bushigwamala, Mwamagigisi, Mkula vilivyopo katika wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Profesa Muhongo anafanya ziara katika mikoa ya Simiyu, Tabora na Shinyanga lengo likiwa ni kukagua miradi ya umeme vijijini pamoja na kuzungumza na wananchi.
Alisema kuwa wakandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na REA awamu ya pili kwa kushirikiana na Tanesco wanatarajiwa kukamilisha na kukabidhi miradi yao mwishoni mwa mwezi Juni ambapo itakuwa ni mwisho wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Profesa Muhongo alisema kuwa mara baada ya kumalizika kwa mradi wa umeme vijijini awamu ya pili, mapema Julai Serikali inatarajia kuingia katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa usambazaji wa nishati ya umeme vijijini lengo likiwa ni mwendelezo wa kuboresha maisha ya wananchi hasa waishio vijijini na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa nishati ya umeme katika ukuaji wa uchumi wa nchi, Serikali imeelekeza nguvu zake zote katika kusambaza umeme husasan vijijini kwa lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia 75 ya watanzania wanapata umeme wa uhakika na hivyo nchi kutoka katika kundi la nchi masikini duniani na kuwa nchi yenye kipato cha kati.
Akizungumzia gharama ya uunganishaji wa umeme nchini kwa wananchi waliopo chini ya mradi wa usambazaji wa umeme vijijini unaotekelezwa na REA Profesa Muhongo alisema kuwa ni shilingi 27,000 ambayo ni VAT peke yake na kuwataka wananchi walio chini ya mradi huo kuchangamkia fursa ili waweze kufaidi umeme kwa gharama ambayo ni ya chini mno.
Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi hasa waishio vijijini wanamudu gharama ya kuunganishiwa umeme na kujikwamua kiuchumi.
Alisisitiza kuwa kwa wananchi waliochelewa kutuma maombi yao ili kuunganishiwa umeme chini ya mradi wa REA awamu ya pili, wasubiri awamu zingine zinazofuata, au walipe shilingi 177,000 kwa Tanesco na kuunganishiwa umeme muda wowote watakaohitaji
“ Kwa wale wanaohitaji kuunganishiwa umeme muda wowote na Tanesco nje ya kutegemea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa na REA kwa awamu watatakiwa kulipa shilingi `177,00 bila nguzo na fedha hizi zinaweza kulipwa kwa awamu, ‘’ alisema Profesa Muhongo.
Aliendelea kufafanua kuwa awali wananchi walitakiwa kulipa shilingi 467,000 lakini Serikali ikaamua kushusha bei hadi kufikia shilingi 177,000 ili kuwawezesha wananchi wote kuunganishiwa umeme.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini awamu ya tatu, Profesa Muhongo alieleza kuwa maombi yatachukuliwa nchi nzima kwa vijiji vilivyokosa umeme katika awamu ya pili, na baada ya hapo mradi utaanza kutekelezwa kwa vijiji vichache kwa kila mkoa, kwa awamu tofauti lengo likiwa ni kuhakikisha panakuwepo na usawa katika kunufaika na miradi ya umeme vijijini.
Akizungumzia gharama ya umeme nchini Profesa Muhongo alisema kuwa gharama za umeme zinatarajiwa kushuka mara baada ya Tanesco kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia
Alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 542, na kuanza kuzalisha gesi, kutapelekea kushuka kwa gharama za umeme kwani umeme unaozalishwa na gesi ni nafuu kuliko umeme unaozalishwa kutokana na mafuta mazito unaotumika sasa.
Aliongeza kuwa mbali na bomba la gesi kuchangia kushuka kwa gharama za umeme na kupatikana kwa umeme wa uhakika, gesi hiyo itapelekea kuongezeka kwa fursa nchini za uwekezaji nchini husan viwanda vya mbolea, sementi na kuongezeka kwa ajira
Alisema kuwa gesi hiyo itatumika katika magari na kupikia majumbani hivyo kupunguza uharibifu wa mazingira.
Akielezea mikakati mingine ya serikali katika kuhakikisha kuwa umeme unaopatikana unakuwa ni wa uhakika, Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imebuni vyanzo vingine ya nishati ya umeme kama vile makaa ya mawe, jua, jotoardhi, bayogesi na upepo huku ikikaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inakuwa ni ya uhakika.

Chapisha Maoni

0 Maoni