Unordered List


RIDHIWANI KIKWETE:SITAKI KUWA SEHEMU YA MBUNGE PAMBIO,NITAHAHAKIKISHA NATATUA KERO ZILIZO NDANI YA UWEZO WANGU

unnamed
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa jimbo la Chalinze ,Bagamoyo mkoani Pwani ,Ridhiwani Kikwete amesema hakugombea nafasi ya ubunge ili kuwa sehemu ya mapambio  bali aliitaka nafasi hiyo ili kuwa sehemu ya suluhisho katika kutafutia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Chalinze.Alisema kiongozi aliyeomba ridhaa ya uongozi kwa wananchi anapaswa kutimiza ahadi alizozitoa na kutatua yale ambayo yapo ndani ya uwezo wake .Aliyasema hayo juzi,katika kijiji cha Changalikwa na Ng’andi kata ya Mbwewe,Bagamoyo wakati akiendelea na ziara yake ya siku kumi anayoifanya kutembelea kata mbalimbali jimboni hapo kujua kero za wananchi na kueleza yale aliyoyatekeleza na kuyachukulia hatua pamoja na kuwashukuru wananchi kwa kuichagua CCM katika chaguzi zilizopita za sekali ya mitaa,vitongoji na vijiji.Ridhiwani alisema hayo baada ya kutolewa malalamiko hususan ya maji na kiafya yanayowakabili kwa kiasi kikubwa wakazi wa kijiji cha Ng’andi na Changalikwa.

Wakazi hao walisema wanakabiliwa na tatizo la maji ambalo linawasababishia kutumia maji ya kwenye mabwawa ambayo hayana usalama katika afaya za watu na kufuata maji umbali wa km zaidi ya 5 huku wakinunua dumu la maji kwa kiasi cha sh.500 hadi 700.
Kufuatia kero hizo Ridhiwani alieleza kuwa hatotaka kuona anakuwa sehemu ya pambio katika uongozi wake lakini atahakikisha anatatua kero  kwa wananchi na kushirikiana nao kwa pamoja kwa lengo la kupata suluhisho la kero hizo.
Ridhiwani alisema kwasasa anafanya taratibu ya kumpeleka waziri wa maji ili aweze kwenda kutembelea maeneo yenye kero kubwa ya maji katika kata ya Mbwewe hadi kata ya Kibindu, kujionea hali halisi ya uchungu wanaoupata wananchi.
Alieleza taarifa alishazifikisha kwa waziri husika na anaamini atafika katika maeneo hayo ili aende kujua ukubwa wa tatizo hilo hatimae kulipatia ufumbuzi na kuwaondolea changamoto hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inawapa usumbufu wakinamama  ambao wanatembea umbali mrefu kufuata maji.
“Nataka kusema kwa undani kwa nguvu tunayokwenda nayo na nyie wananchi kutafutia ufumbuzi matatizo mbalimbali mnayoyapata,naamini waziri atakuja  na atatusaidia kero hiyo “alisema Ridhiwani.
Ridhiwani alisema atahakikisha kuyatekeleza yaliyo ndani ya uwezo wake aliyoyaahidi katika muda mfupi wa uongozi wake ,na aliwaomba wananchi kumkumbusha pale anaposahau na kushirikiana nae ili waweze kupiga hatua ya kimaendeleo.
Alisema tayari alishakaa na viongozi wa mamlaka ya maji na kuzungumza nao  ambapo waliahidi kupatiwa maji kwa kujengewa vioski vitatu vya maji ambapo kimoja kitakuwa katika eneo la shule Changalikwa na viwili vitakuwa vijijini  na kukamilisha tanki kubwa la maji lililopo Mbwewe  ili kupeleka maji maeneo mbalimbali.
Aidha alisema serikali bado inaendelea na hatua za kutatua kero hiyo ambapo inachukua hatua ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu na  kuendelea na awamu ya tatu ya mradi wa maji wa WAMI ambao utasaidia kutatua kero ya maji jimboni hapo.Akizungumzia suala la tatizo la kiafya matika maeneo ya Kibindu na Mbwewe Ridhiwani alieleza kuwa anaendelea kuzungumza na idara husika kuangalia namna ya kujazia watumishi wa afya katika maeneo yenye upungufu mkubwa na kupanga mikakati ya kujenga zahanati katika maeneo ambayo yana ukosefu wa huduma hiyo ili kuwaondolea adha  wananchi wanaotembea umbali mrefu kufuata huduma za kiafya.
Ridhiwani hadi sasa alishatembela kata 3 za Kibindu,Mbwewe na Ubena kwa kutembelea vijiji vinne kwa siku katika kila kata.

Chapisha Maoni

0 Maoni