Unordered List


VIGOGO WIZARA YA UJENZI WAMKIMBIA MAGUFULI!

Waziri ya Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli.
Stori: Makongoro Oging’ na Harun Sanchawa/UWAZI
Baadhi ya vigogo katika Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na Dk. John Pombe Magufuli (pichani), wameikimbia wizara hiyo na kwenda sehemu nyingine kwa kile walichodai ni uongozi wa kibabe na unyanyasaji katika idara ya usalama barabarani na mazingira.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu wizarani hapo umebaini kuwa katika idara hiyo inayoongozwa na Julius Chambo kama Kaimu Mkurugenzi imekimbiwa na vigogo watatu, Juma Kijavara, Omari Kinyange na Samson Nkundineza ambao wameondoka wizarani hapo ndani ya mwezi mmoja, Desemba mwaka jana.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya wizara hiyo vinadai kwamba tangu Chambo ahamishiwe katika idara hiyo akitokea kituo cha mizani Himo mkoani Kilimanjaro, utendaji wa kazi umekuwa ukisuasua kwa kile kinachodaiwa kuwa ni uongozi wa kidikteta pia wameona kama amewekwa hapo kiupendeleo kwa vile mambo ya utawala hajui.

Katika idara hiyo inayoongozwa na Chambo ilikuwa na wahandisi wanne lakini baada ya kuondoka kwa hao watatu alibakia mmoja na inasemekana wameletwa wengine kufidia walioondoka.
Kuhama kwa vigogo hao kumewatia hofu wafanyakazi waliobaki na inasemekana kuwa baadhi yao wanataka kuondoka.

Aidha baadhi ya wafanyakazi wamelalamikia kipindi kirefu alichopewa kukaimu nafasi hiyo. 
“Huwezi kukaimu ofisi kwa muda mrefu namna hiyo hapa kuna tatizo,” alisema mhandisi mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.

Aliongeza kuwa kama wizara haitafanya mabadiliko stahiki kuna wahandisi watatu wataondoka hivyo wizara kupoteza wataalamu wazoefu kitu ambacho kitaleta shida kubwa wizarani hapo.
Gazeti hili lilipomtafuta Chambo ofisini kwake alikiri kuondoka kwa vigogo hao na akadai kuwa ni mmoja tu ndiye aliyemuaga lakini wengine hawakufanya hivyo.

“Mimi naamini wameondoka kwenda kutafuta maslahi zaidi, kuhusu madai mengine mimi siwezi kuzungumzia masuala ya wizara, nendeni kwa katibu mkuu,” alisema Chambo. Naye katibu mkuu wa wizara hiyo, Musa Lyombe alipohojiwa alisema wafanyakazi hao wameondoka Desemba mwaka jana lakini hata yeye ameshangazwa na kuondoka kwao.

“Nafikiri kuna jambo na kuna umuhimu wa kulichunguza suala hili kwa karibu, wao walikuja kwangu nikijua wanafuata maslahi, kwa nini itokee katika idara hiyo moja?” alihoji.

Chapisha Maoni

0 Maoni