Unordered List


BABA MTAKATIFU AJITABIRIA KUFIKIA MWISHO

Papa Fransis.
AKIWA katika maadhimisho ya kuanza mwaka wa pili wa utume wake katika kuongoza Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis, ametoa kauli kuashiria kuwa huenda asidumu katika wadhifa huo kwa muda mrefu ujao.
Alisema hayo juzi katika mahojiano ya ana kwa ana na kituo kimoja cha televisheni cha Mexico, Televisa News, baada ya kutangaza kuwa Desemba mwaka huu, Kanisa Katoliki litaadhimisha Mwaka Mtakatifu.
Mwaka huo Mtakatifu utaanzia Desemba 8, mwaka huu na kuisha Novemba 20, mwakani. Inaelezwa kuwa kuzinduliwa kwa Mwaka Mtakatifu au Jubilee, kunaendana na maadhimisho ya 50 ya kufungwa kwa Baraza la Pili la Vatican, ambalo hukusanya maaskofu ambao huzungumzia mambo ya baadae ya kanisa.
Mwaka huo Mtakatifu utakuwa wa 29 tangu utaratibu huo ulivyoanza mwaka 1300. Kwa kawaida Mwaka Mtakatifu huadhimishwa kila baada ya miaka 25.
Ukomo wake Katika tamko hilo, Baba Mtakatifu Francis mwenye umri wa miaka 78, ameweka wazi kuwa hataadhimisha miaka mingine mitakatifu katika siku zijazo. “Nina hisia kwamba utume wangu utakuwa wa muda mfupi, kama miaka minne au mitano; sijui inaweza hata kuwa miwili au mitatu lakini miaka miwili imeshapita,” alitabiri katika mahojiano hayo.
Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi kama atafuata nyayo za mtangulizi wake, Baba Mtakatifu mstaafu Benedict XVI, ambaye ameweka historia ya kuwa Baba Mtakatifu wa kwanza kustaafu katika miaka 600 iliyopita, baada ya kuchukua hatua hiyo mwaka 2013.
Alipoulizwa swali mahususi kama atafuata nyazo za Baba Mtakatifu mstaafu, Benedict XVI, alijibu; “Huenda Benedict XVI akabakia kuwa Baba Mtakatifu mstaafu pekee kwa miaka mingi ijayo, na huenda akapata mwenzake,” na kuongeza kuwa Baba Mtakatifu mstaafu “ameonesha njia.” Hii si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Francis kuzungumzia ukomo wake, kwa kuwa amewahi kusema kustaafu kwa Baba Mtakatifu Benedict XVI mwaka 2013, kusichukuliwe kuwa tukio la pekee.
Pia, alisema hakuchukia kuteuliwa kuwa Baba Mtakatifu, lakini aliweka wazi kwamba katika wadhifa huo, amejikuta akipoteza uhuru wake. “Natamani tena kuwa na uwezo wa kutoka nje siku moja bila mtu yeyote kunifuatilia na kunitambua nikajinunulie mahitaji yangu,” alisema na kutabasamu.
Lengo la mahojiano hayo na kituo hicho cha Televisa News, lilikuwa kujadili maisha yake ikiwemo mawasiliano yake na baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakimwandikia barua kumshirikisha katika huzuni zao na kupata ushauri wake.
Umasikini, wahamiaji Baba Mtakatifu pia alizungumzia hali ya uhamiaji duniani na kuibuka kwa wimbi la wakimbizi wanaokimbia umasikini, njaa na vita katika nchi zao za kuzaliwa.
Katika mahojiano hayo yaliyochapishwa katika kurasa 17, Baba Mtakatifu Francis alisema kwa kuwa yeye ni Baba Mtakatifu wa kwanza kutoka Bara la Amerika ya Kusini, analazimika kuzungumzia wahamiaji na watu masikini kwa sababu babu zake walihama kutoka Italia kwenda Argentina kutafuta kazi.
“Watu wamekuwa wengi bila kazi, kiasi cha kulazimika kutafuta kazi mahali pengine,” alisema Baba Mtakatifu Francis, ambaye safari yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alitembelea kisiwa cha Lampedusa, Italia kutoa heshima kwa maelfu ya wahamiaji waliokufa wakijaribu kwenda katika Bara la Ulaya. CHANZO: HABARI LEO

Chapisha Maoni

0 Maoni