Unordered List


RAIS WA NIGERIA AAPA KUFA NA BOKO HARAMU


Rais Goodluck Jonathan
Rais Goodluck Jonathan
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan amesema ana matumaini kuwa wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu wa Boko Haram watafurumushwa kutoka kwenye miji na vijiji wanavyovidbihiti, katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.
Rais Jonathan ameitoa kauli hiyo leo katika mahojiano yaliyorushwa na Kituo cha Utangazaji cha Uingereza, BBC, wakati ambapo kundi la Boko Harama likiwa limewaua watu 11 kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo. Watu walioshuhudia wamesma wanamgambo wa Boko Haram wameshambulia mji wa Gamboru uliko kwenye jimbo la Borno, Nigeria.
Wakaazi wa mji wa Fotokol ulioko kwenye mpaka wa Cameroon na Nigeria, wamesema shambulizi hilo limefanyika siku ya Jumatano, mwezi mmoja baada ya Gamboru kutwaliwa tena na majeshi ya Chad, ambayo ni sehemu ya operesheni ya kijeshi iliyoanzishwa na mataifa manne ya kanda hiyo, dhidi ya Boko Haram.(P.T)
Mkuu wa vikosi vya Niger katika operesheni za kupambana na Boko Haram, Kanali Toumba Mohamed, anasema walikuwa na wakati mgumu wakati wa kupambana na kundi hilo. ''Tulikabiliana na adui ambaye kweli alikuwa amelidhibiti eneo hili na halikuwa jambo rahisi kumuondoa, lakini tumefanikiwa na nguvu za huyu adui zimepungua,'' alisema Kanali Mohamed.
Mudi Dankaka mkaazi wa Fotokol, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba wanamgambo wa Boko Haram waliuvamia mji wa Gamboru ulioko mpakani mwa Nigeria na Cameroon, wakiwa katika pikipiki na kuwaua watu wanane siku ya Jumatano. Dankaka, amefafanua kuwa watu wengine watatu waliuawa jana Alhamisi. Shambulizi hili linaonekana kama changamoto kubwa zinazoikabili Nigeria wakati ikielekea kufanya uchaguzi wake mkuu hapo Machi 28, mwaka huu.
Mwezi uliopita, majeshi ya Chad yalipongezwa kwa kuukomboa mji wa Gamboru kutoka kwa Boko Haram, lakini hatua ya majeshi hayo kuondoka Nigeria wiki iliyopita, inaonekana kuuacha mji huo bila ulinzi wowote kutoka kwa majeshi ya Nigeria.
Operesheni ina lengo la kuliteketeza kundi la Boko Haram
Operesheni ya pamoja ya majeshi ya Chad, Nigeria, Cameroon na Niger ni sehemu ya lengo la kuliteketeza kabisa kundi la Boko Haram ambalo limekuwa likiendesha operesheni zake kwa miaka sita sasa. Siku ya Jumanne, jeshi la Nigeria lilisema kuwa limewafurumusha wanamgambo wa Boko Haram kutoka kwenye wilaya zote za kaskazini-mashariki.
Shambulizi la Gamboru limefanyika baada ya kutolewa taarifa za ukatili mwingine uliofanywa na Boko Haram katika mji wa Bama, ulioko pia kwenye jimbo la Borno. Kundi hilo liliwachinja wanawake kadhaa ambao walilazimishwa kuolewa na wanamgambo wake. Watu walioshuhudia wamesema magaidi hayo walifanya ukatili huo, wakisema hawawezi kuwaruhusu wake zao waolewe na wanaume makafiri. Msemaji wa usalama wa ndani wa Nigeria, Mike Omeri, alisema atajaribu kuthibitisha kuhusu taarifa hizo.
Ama kwa upande mwingine, balozi za Marekani katika mataifa ya Afrika Magharibi ya Niger na Mali, zimeimarisha usalama wa wanadiplomasia wake pamoja na familia zao, huku kukiwa na wasiwasi wa nchi hizo kushambuliwa na wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu, wakiwemo Boko Haram.
Hatua hiyo inatokana na shambulizi la kigaidi lililofanywa Machi 7 kwenye mkahawa mmoja huko Bamako uliokuwa na raia wengi wa kigeni, pamoja na mashambulizi yaliyofanywa na Boko Haram nchini Niger.
Kundi la Boko Haram ambalo linaendesha shughuli zake kaskazini mwa Nigeria, limekuwa katika vita na Nigeria na mataifa jirani tangu mwaka 2009 na limesababisha mauawaji ya zaidi ya watu 13,000.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE,RTRE,APE-DW

Chapisha Maoni

0 Maoni