Unordered List


BUMBULI WABARIKI URAIS WA JANUARY MAKAMBA,WASEMA NI SHUJAA WAO


Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Naibu Waziri Sayansi na Teknolojia, January Makamba akipokelewa na wazee mara baada ya kuwasili jimboni kwake.
Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Naibu Waziri Sayansi na Teknolojia, January Makamba akipokelewa na akina mama na kupewa baraka zake.
Na Raisa Said, Bumbuli.
Wakazi mbalimbali wa Jimbo la Bumbuli, wilayani Lushoto, Mkoani Tanga wamesema kuwa wapo tayari kumuunga mkono Mbunge wa Jimbo hilo, January Makamba kama ataamua kuwania nafasi ya kuwa mgombea wa Uraisi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu. Wakazi hao ambao walionyesha nia yao hiyo katika sehemu mbalimbali alizopita Mbunge huyo katika ziara yake ya siku sita kutembelea jimbo lake iliyoanza Machi 30. Makamba ni mmojawapo wa watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya Urais.
Alipokuwa katika kata ya Tamota, viongozi wa dini walimfanyia maombi maalum ambayo yaliongozwa na Mchungaji Amasia Mweta na Sheikh Amiri Yahaya Shekibula mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutumbiwa na Mbunge huyo kijana. Akihutubia mamia ya wakazi wa Bumbuli katika maeneo yote aliyopita kwenye ziara yake, Makamba aliwashukuru wakazi wa jimbo hilo kwa kumchagua kuwa Mbunge wao na kusema kama sio wao asingeweza kuonekana na kutajwa katika kuwania nafasi ya kuwa mgombea wa CCM.
Makamba, huku akishangiliwa na wakazi hao wa maeneo hayo, alisema kuwa hakuna namna ambayo unaweza kutengeneza watu kukutaja katika nafasi za juu bila kupitia kwa wananchi kukuchagua katika nafasi ya kuwawakilisha. "Kutajwa si dhambi na kwa kuwa fomu za uchaguzi sio sumu si dhambi pia kuchukua na kuingia katika kinyang'anyiro hicho," alisema na kuongeza kuwa sasa hivi kuna kiu kubwa ya uongozi wa aina mpya na kuna watu wamemuona na kumtaja yeye jambo ambalo si baya.
Nao wananchi , wakiwemo vijana, kina mama na wazee katika maeneo mbalimbali aliyopitia Makamba, walimhakikishia Mbunge huyo kuwa hivi sasa hawatampokea mtu yeyote ambaye atakuja kujipitisha katika jimbo hilo hadi hapo watakapojua hatma ya utekelezaji wa nia ya Mbunge huyo kuwania nafasi ya kuwa mgombea wa Urais kupitia CCM. Nao waumini wa Usharika wa Bumbuli walimtaja Mbunge huyo kuwa jasiri, mweledi na mwenye maono mapana na wakasema wanaahidi kuwa bega kwa bega katika harakati hiyo ya kuwania kuwa mgombea wa CCM.(Muro)

Chapisha Maoni

0 Maoni