Unordered List


MTEMI SYLVESTER YAREDI; WATANZANIA WASIZUIWE KWENDA DODOMA.

Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Taifa Viti Vitano Bara, Mtemi Sylvester Yaredi akizungumza na Waandishi wa Habari.



TAMKO LA KULAANI KAULI YA MKUU WA MKOA WA MWANZA BWANA STANSLAUS MAGESSA MULONGO.


Ndugu wanahabari,

Kwanza nikushukuruni kwa kuitikia wito wangu na kukubali kuja kuungana nami ili kupitia ninyi Watanzania wajue hasa wale Watanzania wenzangu wanaotokea Mkoa wa Mwanza.

Siku ya jana binafsi nilishtushwa mno na kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza eti akitoa maelekezo kwa Kamanda wa Polisi kuzuia watu kwenda Dodoma. Ni imani yangu kuwa si mimi peke yangu bali Watanzania wengi watakuwa wameshangazwa na kauli ya Magessa. Ambayo kimsingi ni kuvunja Katiba ya nchi ambayo yeye amepa kuilinda na kuitetea na ni kauli ya ajabu sana kutolewa na mtu mwenye nafasi nyeti kama yake.

Nafasi aliyonayo ni kumwakilisha Raisi hapo Mwanza hivyo vile vile sitaki kuamini kwamba amefikia hatua ya kutoa kauli ambazo Watanzania tutaishia kujiuliza maswali mengi hasa tukitaka kujua ni nani hasa aliyemtuma manake haiwezekani mtu aliyeaminiwa na Raisi kutoa kauli ya vitisho na yenye kila maana ya kuvunja Katiba ya Nchi jambo ambalo naomba wenzangu kusimama pamoja nami na kulaani kauli hiyo kwa namna yeyote inayofaa. Hili ni Taifa letu sote hivyo asitokee mtu akadhani kwamba yeye ni zaidi ya Watanzania wote ama yeye ni juu ya Katiba na Sheria za Nchi na kujiamulia kututisha atakavyo.

Ndugu Wanahabari,

Katiba yetu ya mwaka 1977 katika Ibara yake ya 17(1) iko wazi kabisa nanukuu;
“Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.”

Hivyo ndivyo Katiba inavyotamka kwamba kimsingi Mtanzania kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni haki yake Kikatiba. Sasa leo ni lazma Magessa atueleze yeye ni kama nani hata kuzuia Watanzania kutimiza haki yao hiyo ya Kikatiba. Na labda kama ni mgeni lazma ajue Watanzania hasa wana CCM unapofikia wakati kama huu wengi wao wanakuwa na shauku ya kwenda Dodoma si tu kwenda kujumuika na wenzao katika kushuhudia moshi mweupe ukitoka katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM bali pia kufurahi na kujifunza namna chaguzi, mapendekezo na hata namna ambavyo vikao vinaendeshwa ndani ya CCM.

Hili halijaanza leo na wala halitazamiwi kuisha leo ama kesho kwa vitisho vya namna hiyo labda Katiba iseme vinginevyo. Kauli za namna hii ni za kugawa Wananchi na vile vile ni za kuhatarisha Uhuru na Haki zetu kama Watanzania ambazo Viongozi wetu wamekuwa wakizisimamia kwa umakini mkubwa mno. Ni wazi kwamba kama kulikuwa na tatizo lolote Vyombo vyetu vyenye dhamana ya kusimamia Ulinzi na Usalama vingeona hayo na basi wao ndio wangekuwa na Jukumu la kutoa kauli za namna hiyo na hasa vyombo vilivyoko Dodoma.

Ndugu Wanahabari,

Vitisho vya namna hii na kauli za namna hii ni lazma vitawaweka Watanzania njia panda na kuishia kujiuliza maswali bila majibu ya kwamba ni kwa nini yote hayo. Na ni kwa nini kauli hiyo itolewe wakati huu. Lakini imekuwa ajabu kweli kweli kwamba katika Mikoa 31 tuliyo nayo ametokea Mkuu wa Mkoa mmoja tu aliyetoa kauli ya ajabu isiyo stahiki kabisa kutolewa na mtu wa namna yake.

Bwana Magessa amekuwa na tabia zake za peke yake tokea akiwa Arusha hivyo ni lazma sasa ngazi za kinidhamu ambazo bwana Magessa anawajibika kwazo zione namna ya kushughulika naye kabla hajaendelea kuwagawa Watanzania kwa kauli zisizo na staha. Haya mambo hayavumiliki hata kidogo. Watanzania na hasa wana CCM waachwe waende Dodoma manake kwanza kwa kufanya hivyo mji wa Dodoma nao utakuwa na mengi ya kunufaika kupitia ugeni huo.
Lakini vile vile mshikamano wa Watanzania unaendelea kukomaa na watu wanaendelea kufahamiana. Binafsi sina shaka hata kidogo na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama na ndiyo maana wamekaa kimya kwa kuwa wamejipanga na wanajua Watanzania si watu wa fujo ila wanapenda kushuhudia na kusimamia haki zao za msingi. Na niseme tu kauli zingine hizi hupelekea kuchochea watu manake hata wale ambao hawakuwa na nia ya kwenda Dodoma sasa wataenda ili kushuhudia ni kwa nini wanazuiwa.
Ndugu Wanahabari,
Nalaani kauli hiyo kama Sylvester Yaredi na niendelee kuwaomba wale wenye mapenzi mema na Taifa hili waungane nami katika kulaani kitendo hicho na hasa baada ya kumwangalia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na kutoridhishwa kabisa na kauli yake yenye nia ya kututisha pasi sababu ya msingi; Dodoma tutakwenda ili kushuhudia Chama chetu kinavyoendesha vikao vyake na si hivyo tu, bali tunakwenda vile vile ili tuweze kurudi na Jina la Raisi atayepokea mikoba ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Nimalizie hivi aliwahi kusema Johann Wolfgang “The Coward only threatens when he is safe.”

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Imeandaliwa na;
Mtemi Sylvester Yaredi
(Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Taifa Viti Vitano Bara – Mwanza)

Na Sufyan Omar

Chapisha Maoni

0 Maoni