Unordered List


WAZIRI MKUU KUKUTANA NA WAFANYABIASHARA SOKO LA SABASABA MKOANI DODOMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameahidi kukutana na wafanyabiashara wa soko la Sabasaba mkoani Dodoma ili kuzungumzia namna ya kulikarabati na kulifanya liwe la kisasa.

Amesema miongoni mwa mambo watakayoyajadili katika kikao hicho ambacho hakutaja siku ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara hasa kwa wanaouza bidhaa nje ya maduka.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 5, 2016) wakati alipotembelea maduka hayo yaliyoko katika barabara ya One Way inayopita katikati ya barabara ya sita hadi ya 11 pamoja na soko la Sabasaba akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.

Amesema Serikali tayari imeshahamia Dodoma hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kutumia fursa hiyo kwa kuboresha biashara zao ili waweze kumudu ushindani wa soko.

“Wafanyabiashara lazima mboreshe biashara zenu, muongeze usafi zaidi na ikiwezekana muimarishe majengo yenu yawe ya kisasa zaidi kwani haiwezekani maduka ya Makao Makuu ya Nchi yawe katika hali hii,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara hao wasiogope kwenda kukopa katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa lengo la kujiongeza mitaji na kupanua biashara.

Amesema tayari alishatoa maagizo kwa wamiliki wa benki kuhakikisha wanawawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwapa mikopo, hivyo aliwataka wasiogope na badala yake wachangamkie fursa hiyo. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea Mtaa wa One Way mjini Dodoma Oktoba 5, 2016. 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitembelea eneo maarufu la biashara mjini Dodoma la Sabasaba Oktoba 5, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa soko hilo.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia moja ya nguo ya mtumba alipotembelea soko hilo la Sabasaba Mkoani Dodoma Oktoba 5, 2016.

Chapisha Maoni

0 Maoni