Unordered List


SHAKA ATAKA WACHAPAKAZI WABAKI MAKAO MAKUU UVCCM



Na Mwandishi Wetu,

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka watendaji na watumishi wa Makao Makuu ya jumuiya hiyo  kuanza kujipima, kujitathmini na kujipanga upya kimamakati  kwa sababu muda wa  kupiga maneno haupo ila  vinavyohitajika ni uwezo binafsi  na vitendo.

Pia umoja huo umewasisitiza watendaji , wahudumu na watumishi wa jumuiya hiyo kuongozwa na msingi ya nidhamu, uwajibikaji kazini na kuacha tabia za mzaha na masikhara wakati wa kazi.

Kaimu Katibu Mkuu  UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka alitoa maelezo hayo jana alipokutana  na kufanya kikao na watumishi wa UVCCM  Makao Makuu  kwa ajili  kutathmini utendaji wa jumuiya kwa mwaka 2016 na kupanga mikakati ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka  2017.

Shaka alisema  pamoja na kusikiliza michango , maoni , ushauri , mawazo na changamoto zinazowakabili watumishi na namna ya kuzitatua kwa mwaka 2017  lazima uwe mwaka  wa vitendo na mafanikio.

"Tutabadili kila kona yenye kasoro au dosari , lengo si kukomoana ila ni katika kujipanga tena upya, asiyeweza aseme hawezi ili akae kando , kama mtu  hajimudu hatapewa dhamana yoyote kwasababu ya ushikaji na urafiki "Alisema Shaka.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema makao makuu inahitaji kuwa kama kioo, sifa ya kioo ni kujiona na kujitambua, kama umechafuka jisafishe ili uwe nadhifu na makini bila mtu  kusukumwa.

Alisema kila aliyepangiwa kazi yake aifanye kwa  mujibu wa hadidu za rejea na maelekezo ya kikanuni hivyo asiyetaka kujituma na kutimiza wajibu wake atakuwa haitakii mema jumuiya na hivyo hatavumiliwa na kutazamwa.

"Tukijipanga vyema hapa Makao Makuu, kila mmoja akatimiza wajibu wake naamini mambo yakaenda kama inavyotakiwa, hakuna urasimu wala njoo kesho, wenzetu wilayani na mikoani watatueheshimu, tukiwatuma watatumika na kutupatia majawabu chanya "Alieleza

Hata hivyo Shaka  aliwataka wana  jumuiya mahali popote  walipo nchini wajione  na kujihesabu wao ni ndugu wa tumbo moja, wapendane, wasikubali kukaribisha majungu au hasama kwasababu zama hizo zimepita na hazitarejea tena.

Pia aliwakumbusha watendaji hao wa makao makuu kutunza siri za ofisi, nyaraka muhimu ikiwemo na kujiandaa vyema  kufanikisha uchaguzi Mkuu ujao  kwa mujibu wa taratibu, kanumi na katiba ya ccm.

"Ukipewa jukumu la kusimamia tenda haki, timiza wajibu wako bila upendeleo, ukiharibu na kuvurunda utaadhibiwa bila huruma na si hasha ukajifukuzisha kazi mwenyewe kwa ukiukaji wako wa  maadili na kanuni ya utimishi"alisisitiza Shaka .

Kaimu huyo Katibu Mkuu alimsifu na kuwashukuru Mwenyekiti wa UVCCM sadifa Juma Khamis, Makamo Mwenyeliti   Mboni Mhita , manaibu makatibu wakuu wake, wakuu wa idara na watendaji wote  wa  jumuiya hiyo kwa kumpa ushirikiano katika kutimiza majukumu  na kuifanya jumuiya yao kuendelea kukamilisha mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutawala.

Chapisha Maoni

0 Maoni