Mheshimiwa Dkt. Augustine P.
Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
na Mwenyekiti wa SADC wa Kamati ya Mawaziri ya Asasi ya Ushirikiano wa
Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Ministerial Committee of the Organ on
Politics, Defense and Security Cooperation – MCO) amewasili Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa ajili ya kuongoza Ujumbe wa Mawaziri wa
Mambo ya Nje wa SADC Troika (Tanzania, Angola na Msumbiji) kwa dhumuni
la kufanya Misheni ya Pili ya kutathmini hali ya siasa, ulinzi na
usalama nchini humo.
Misheni hii inafanyika
kufuatia Azimio la Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC Troika
Mbili uliofanyika Falme ya Swaziland tarehe 17 Machi, 2017. Mkutano huo
uliagiza kufanyika kwa Misheni ya Pili ili kuendelea kufuatilia kwa
ukaribu maendeleo ya hali ya siasa nchini DRC wakati ikifanya maandalizi
ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba, 2017.
Sambamba na hayo, Viongozi
Wakuu katika Mkutano huo walipokea na kujadili taarifa ya hatua
zilizochukuliwa na SADC katika kutatua changamoto za kisiasa, kiulinzi
na kiusalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwemo Taarifa ya
Misheni ya Kwanza ya Mawaziri iliyofanyika mwezi Oktoba, 2016 na Taarifa
ya Misheni ya Timu ya Wataalam wa SADC nchini DRC iliyofanyika mwezi
Februari, 2017.
Katika Misheni hii ya Pili,
ujumbe wa Angola utaongozwa na Mhe. Manuel Augusto, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje; na ujumbe wa Msumbiji utaongozwa na Mhe. Nyeleti Mondlane,
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Ratiba inaonyesha kuwa ujumbe
wa Misheni ya Mawaziri wa SADC utakutana na kufanya mazungumzo na wadau
wafuatao: Serikali ya DRC akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo;
Wawakilishi wa Jeshi la Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO);
Wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini DRC (CENCO);
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa na Asasi za Kiraia; na Ofisi ya Rais –
DRC. Aidha, Mawaziri watapata pia fursa ya kufanya mazungumzo na
Mabalozi wa nchi wanachama wa SADC wenye makazi mjini Kinshasa.
Misheni inatarajiwa kukamilika tarehe 21 Aprili, 2017.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
19 Aprili, 2017
0 Maoni