Serikali kupitia Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kushughulikia
suala la huduma za afya bure kwa watu wenye ulemavu.
Hayo yamesemwa leo Bungeni
Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla kwa niaba ya Waziri Ummy
Mwalimu.
Akizungumza wakati wa
kipindi cha maswali na majibu kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalum Stella
Ikupa Alex aliyetaka kupata ufafanuzi juu ya suala hilo, Dkt. Kigwangalla
alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kutoa huduma za afya bure kwa makundi
maalum likiwemo watu wenye ulemavu.
“Dhumuni la Sera ya Afya
ya mwaka 2007 ni kuwezesha watu wenye ulemavu wazingatiwe katika makundi maalum
ya watu wanaostahili msamaha utolewao kwa kuzingatia endapo mlemavu huyo hana
uwezo wa kulipia huduma hiyo au awe katika makundi maalum ili kupata huduma
bora za afya kama ilivyo kwa watu wengine,” alisisitiza Dkt.Kigwangalla.
Sera hiyo imeainisha makundi maalum yanayostahili
kupata msamaha wa huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma kuwa ni wazee
wenye umri zaidi ya miaka 60, watoto chini ya miaka mitano,watoto waishio
katika mazingira hatarishi, wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi.
Aliongeza kuwa watu wengine ambao wapo kwenye
makundi maalumu ni wenye magonjwa sugu
kama Kifua kikuu, Ukimwi, Kisukari,
Magonjwa ya Moyo, Pumu, Sikoseli, Ukoma, Saratani na Magonjwa ya Akili.
Aidha alisema kuwa katika
kuweka uwiano sawa kwa Watanzania wote bila ubaguzi Serikali ya awamu ya tano ina pendekezo la
kutoa bima ya afya ya lazima kwa watu wote ambapo utasaidia pia kwa watu wenye
msamaha kupata huduma bora.
Kama Serikali
itapitisha pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa Watanzania wote litasaidia
upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
0 Maoni