Jumatano, 10 Mei 2017

VIJANA NA FURSA ZA UJIO WA RAIS JACOB ZUMA

Kesho kama ilivyoada ya ukarimu, uzuri, umahiri na umashughuli wa nchi yetu tutakuwa na ugeni mwingine tena kutoka nchi ya Afrika ya kusini, nchi ambayo tumeipigania na kumwaga damu yetu ili kuikomboa toka mikononi mwa makabulu wabaguzi wa rangi, watu wa Africa kusini wana deni kubwa na kila sababu ya kufanya kazi na sisi, hii ni katika mfululizo wa ugeni ambao  umekuwa ukitutembelea kila uchwao, kuanzia Rais wa Vietnam, Mfalme wa Morroco, Rais wa Rwanda, Rais wa Uganda, DRC Congo, mpaka Uturuki na wengine wengi kabisa. 

Ni mara zote hawa wakubwa wa nchi za watu wamekuwa wakija na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara wakubwa na wa kati ambao kimsingi hawaji hapa Tanzania kutalii tu maeneo adhimu ya nchi yetu kama mbuga za Serengeti na visiwa vya Zanzibar bali pia kutizama fursa za kiuchumi na ikiwezekana kuingia ubia na wafanyabiashara wa Kitanzania. Hima sisi sote kuanza kushiriki hizi tafrija na kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara.

Tumeshuhudia ziara nyingi za marais wageni wakija hapa nchini pamoja na wafanyabiara wao tangu enzi za rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa William Benjamini Mkapa, na ile ya awamu ya nne ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na hata ya sasa kwenye serikali ya awamu hii ya tano ya Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli lakini tujiulize ni mara ngapi hawa wafanyibiashara wageni wameweza kuingia ubia na hawa wafanyabiashara wa hapa nyumbani? Na kama wameingia nao ubia ni wangapi kati ya mamilioni ya Watanzania? Je ni sawa kuendelea kuwapeleka wafanyabiashara wetu walewale kila siku tupatapo ugeni?

Kwanini basi hatuoni ushiriki mkubwa wa kwenye ziara hizi na hasa upande wa vijana?

Mfumo na utaratibu wa kuchagua watu wanaohudhuria tafrija hizi sio endelevu na jumuishi kwakuwa hautoi nafasi kwa wale wenye mawazo na bado hawajaweza kuji-establish kupata nafasi ya kwenda kuuza mawazo yao ili waweze kupata wabia wa kufanya nao biashara. Ukiangalia kwa umakini mkubwa utangundua kuwa tangu awamu ya Mheshimiwa Mkapa mpaka leo hii awamu ya tano ya Mh Rais Magufuli wanaohudhuria hizi tafrija ni wale wale tu. Sio kweli kwamba eti wajumbe wa TPSF na jukwaa ndogo la biashara ndio wenye uwezo wa kuingia ubia na kila muwekezaji anaetoka nje kila siku, Upo uwezekano wa wafanyabiashara wetu kukataa fursa kadha wa kadha kwakuwa kwao hazina maslahi lakini labda kwetu vijana tungeweza kuzifanyia kazi, hii si sawa.

Nini Kifanyike?

Sasa tunadhani ni wakati muafaka wa vijana kupata nafasi ya kualikwa na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wanaoambatana na Marais wao, sote tunajua kiu ya vijana wetu katika kupigania maendeleo yao Binafsi na ya nchi yao lakini hawapati hizi fursa adhimu sana, nchi yetu ina fursa nyingi sana za maendeleo ya kibiashara ambazo wafanyabiashara wetu wameshindwa kabisa kuziendeleza kwa ukubwa wake na matokeo yake hatuzalishi vitu vya kutosha hapa nchini nakubaki kuagiza vitu toka nje ya nchi. Ni aibu kubwa sisi Tanzania kuagiza bidhaa za vyakula toka nje ya nchi.

Tatizo la kukosa taarifa muhimu juu ya upatikanaji wa masoko na mitaji ya kuendeleza biashara zetu ni kubwa sana kwa vijana wetu, sasa ni wakati muafaka wa kuanza rasmi kuwaalika vijana wanaojielewa wenye mawazo mazuri, walioanza tayari biashara zao lakini wanatafuta wabia wa kufanya nao biashara. Vijana wetu wana ari, nguvu na utayari wa kuhakikisha kwamba dhana nzima ya Tanzania ya viwanda inafikiwa lakini hali inakuwa ngumu kama tunawanyima fursa adhimu kama hizi.

Tumefarijika kusikia kuwa TIC ndio watakuwa waratibu wa wafanyabishara wa kitanzania watakao ona umuhimu wa kukutana na wafanyabiashara watakao toka Afrika ya kusini na Mheshimiwa Rais Jacob Zuma. Hii hatua ni muhimu kwakuwa inaondoa upendeleo na urasimu unaofanywa na hizi taasisi zilizokuwa zikiratibu mfanyabiashara gani aende kuhudhuria hizi tafrija na ndio hao wamekuwa kila uchwao wanapeleka watu wale wale ambao huwa hawana shida, hawana kiu, wala mawazo mapya ya kuzungumza na wageni. Naipongeza serikali kwa kusikia na kuliona hili.

Ni mara nyingi tu tunasikia vijana wanatuma maombi ya kuhudhuria hizi tafrija kupitia hizi taasisi binafsi lakini ni mara zote tunasikia wananyimwa, ni imani yetu kwamba TIC hawatarudia hili kosa.

Pindi ambapo vijana ambao ni wasomi wakianza kufanya biashara ndipo tutakapoona mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kiuendeshaji biashara hapa nchini kwetu, sasa ni vyema tukawapa fursa. Ni jambo linalosikitisha kuona kwamba tangu watoke wazee wetu akina Reginald Mengi, akina Mufuruki, na wazee wenginewe hakujawahi kuwa na vijana wanaofuata kwa karibu kuwa mahiri wa kufanya biashara bali tumeona wengi wakishika nyadhifa kubwa za kisiasa na kuajiriwa tu nchi hii tutaigeuza kuwa soko la wafanyabiashara wageni, na hii haifai. 

Kwa vijana.

Sisi vijana ni lazima tuanze kutafuta fursa mbalimbali zilizopo ndani na nje ya nchi yetu, kuwa na ushirikano na kuaminiana ni nguzo kuu kwenye kutengeneza biashara kubwa. Nadhani sote huwa inatuwia vigumu sana kuona hakuna makampuni ya wazawa yanayofanya vizuri kwenye sekta rahisi kabisa kama ya bima kwa mfano wakati wateja ni sisi sisi, kutokuaminiana, kuchukiana na kutokuwa makini juu ya uendeshaji wa makampuni yetu ndiko kunatufanya tushindwe kupeana fursa sisi kwa sisi. Kampuni inatoka Kenya ama Afrika kusini inaingia leo na baada ya miezi sita inawateja millioni na za wazawa bado zinasuasua lazima kuna tatizo sehemu. 

Kwa kusema hayo basi yatupasa tupeana kazi ili tuweze kusonga mbele daima. Kama kuna watu watabahatika kwenda kwenye hii tafrija basi chondechonde nenda na smart phone yako ama Ipad ili uanzishe mawasiliano palepale, kama kutuma taarifa muhimu na mahsusi kuhusu kampuni yako ama yenu na bila kusahau business cards, deals zingine inafaa zifungwe hata palepale kama sio kuzianzishia mazungumzo pale.

Kwakuwa vijana ndio wachangiaji wakubwa wa nchi yetu basi ni vyema wakapatiwa kipaumbele kwenye kuchangamkia hizi fursa, nchi yetu ina fursa nyingi sana za kilimo, uvuvi wa bahari kuu, huduma za meli, renewable energy na nyingine nyingi sana. Wachaguliwe vijana ambao wamethubutu kuanza biashara na wale wadogo wenye mawazo makubwa sana na uwezo wa kujieleza a ama kuzielezea biashara ama mawazo yao kinagaubaga kwenda nao kujumuika na ugeni huu.

Balozi zetu ziwe kitovu muhimu sana kwenye mambo ya kutafuta taarifa na fursa za biashara na masoko, ni rahisi sana kwa wao kufanya hizi kazi, kwahiyo kuwa na mtu wa bishara ubalozini ambae atakuwa akiitumia vizuri website ya ubalozi wetu wa nchi husika kutupa taarifa muhimu kama za masoko, na wabia wenye mitaji tutasonga mbele kirahisi sana. So kwa afisa bishara wa ubalozini hata kuwa dalali wa kuunganisha biashara za Tanzania na hiyo nchi husika ni sawa tu ili mradi sio Biashara haramu ama utapeli.

Wizara ya mambo ya nje ijitahidi kuitisha makongamano ya kimataifa ya kibishara ambayo sio ngumu kuyafanya hata kwa sekta mojamoja ikiwezekana. Tangu awamu hii iingie tumeshuhudia tukijihusisha sana na utatuzi wa migogoro ya nchi zingine jambo ambalo ni zuri kabisa kabisa ila ni vyema tukatafuta hukohuko pia na fursa mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kutupatia fursa nyingi za biashara na huu ndio mwelekeo wa dunia ya leo ambayo inapenda diplomasia ya kiuchumi.

Vijana amkeni, twendeni mashambani, tuanzishe viwanda vidogo vidogo, tuongeze maarifa juu ya uelewa wetu,tuitumie serikali yetu vizuri kwa kupata taarifa muhimu kuhusu uwekezaji ili tuweze kusonga mbele zaidi. Tuungane na Rais wetu ambaye tayari ameonyesha kuwa na mapenzi makubwa na vijana kwa kuwateua katika nyadifa mbalimbali nyeti za kiserikali. Rais wetu pia ana nia safi kabisa ya kufanya mapunduzi ya kiuchumi kupitia agenda yake kuu ya viwanda ni jukumu letu kuhakikisha liweze kutimia. Narudia, jukumu letu ni moja tu kuikuza nchi yetu kiuchumi kwa kujituma zaidi, kwa hiyo tujitoe na tufanye kazi kwelikweli.

Tumewahi jiuliza viongozi wenzetu vijana katika ngazi za kata, wilaya, mkoa wanashiriki vipi katika kuibua vipaji vipya vya biashara na kuwasihi kushiriki katika kongamano mbalimbali zitakazowasaidia kufunguka macho na kupata fursa? Hatujachelewa bado ni vyema basi tufanye hiyo kazi sasa ya kuhudumia na kuonyesha njia/uongozi kwa vijana wenzetu kwa kasi na ari mpya. Tanzania ni yetu sote. 

Pamoja tuijenge nchi yetu tukufu ya Tanzania. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania. 

Kutoka Idara ya Uhamasishaji Na Chipukizi - UVCCM.
Share:
UVCCM TANZANIA. Inaendeshwa na Blogger.

Mdau Janza fomu hii

Jina

Barua pepe *

Ujumbe *

Followers

Google+ Followers

WANAOPERUZI KWA SIKU

VideoBar

Maudhui haya bado hayapatikani kupitia miunganisho iliyosimbwa kwa njia fiche.

YALIYOMO

Follow us by Email

FAHADI SIRAJI

FAHADI SIRAJI
Mtengenezaji na Msimamizi Mkuu wa Blog hii

WAJUMBE WA BARAZA KUU UVCCM TAIFA

IKO KATIKA MAREKEBISHO

My Blog List

Translate/chagua lugha

MAKATIBU WAKUU WA ZAMANI UVCCM

Kumbukumbu la Blogu