NA MWANDISHI WETU
Rais John Magufuli ameukumbuka
mchango wa marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na
kuwashukuru huku akieleza kuwa wao ndiyo waliotengeneza maisha yake ya
kisiasa hadi kuwa kiongozi.
Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu,
Julai 10 wilayani Chato wakati wa uzinduzi wa nyumba 50 zilizojengwa na
Taasisi ya Mkapa Foundation.
“Nakumbuka siku hiyo tulikuja hapa
Chato na wewe (Mkapa) Msafara ulisimamishwa na ukawaambia wananchi wa
Chato nichagulieni huyu, nakumbuka ulikuwa umevaa viatu vyekundu,”
amesema na kuongeza:
“Kwa bahati nzuri, wananchi wa Chato
wakanichagua, baadaye ukanichagua kuwa naibu waziri. Wewe ulinitangaza,
sikustahili chochote, maneno yako yalikuwa na nguvu kwa Watanzania.”
Amesema anamkushukuru pia Rais
Mstaafu Jakaya Kkwete na kusema: “Baada ya kipindi cha Mkapa, Kikwete
alipokuja, lakini kwanza wewe ukanipitisha kugombea ubunge tena kwa mara
nyingine, nikachaguliwa bila kupingwa katika jimbo hili.” Amesema
Amesema hata katika kipindi cha awamu ya nne, Rais Kikwete alimteua katika wizara mbalimbali.
“Kwangu mimi nyinyi mlitengeneza maisha yangu katika uongozi. Pia
nawashukuru sana viongozi wa awamu ya kwanza, Nyerere na Mwinyi ambao
walitengeneza mazingira mazuri ndani ya Chama cha Mapinduzi,” amesema na
kuongeza:
“Kwangu mimi sina cha kuwalipa jukumu langu ni kuwatetea na
ninawaahidi Watanzania kuwa nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote,
namuomba Mungu asinifanye nikawa na kiburi namuomba asinifanye nikasahau
nilipotoka.”
0 Maoni