Unordered List


HAKUNA MGONJWA ATAKAYEKOSA DAWA-MAJALIWA

lod2
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba hakuna mgonjwa atakayekwenda kutibiwa katika hospitali, vituo vya afya au zahanati  bila ya kupatiwa dawa.
Ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Julai 10, 2017), wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Wilaya.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa katika ziara yake ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, alisema Serikali haitaki kusikia wananchi wanakwenda hospitali, Vituo vya afya au zahanati na kukosa dawa.

Alisema moja kati ya ajenda muhimu ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake, ambapo kila mwezi halmashauri zote nchini zinapelekewa fedha za ununuzi wa dawa.

“Serikali hii ya Rais Dkt. John Magufuli inatoa fedha za kununulia dawa kila mwezi katika halmashauri zote nchini. Sasa kama hapa Liwale kuna malalamiko ya wananchi kukosa dawa katika hospitali yetu, Mkuu wa Wilaya kafuatilie huko Halmashauri ili kujua wanapeleka wapi fedha za dawa.”
Katika bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 236 zimetengwa kwenye ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema hali ya upatikanaji wa dawa muhimu kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 iliongezeka kwa asilimia 50 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2015/2016.

 Bw. Zambi alisema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Februari 2017 mkoa wa Lindi ulipokea sh milioni 538 kwa ajili ya ununuzi wa dawa kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
 “Hospitali ya mkoa ilipokea sh. milioni 195,328,186 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na pia ilitumia sh.  Milioni 127,171,700 toka fedha za uchangiaji kwa ununuzi wa dawa.”

 Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wa Halmashauri kwenda vijijini na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa utunzaji wa mazingira ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
 Pia amewaagiza Maofisa Kilimo wote kuhakikisha wanaacha kushinda maofisini na badala yake waende mashambani kwa ajili ya kuwaelimisha wakulima namna bora ya kulima kwa kufuata njia za kisasa ili kupata tija.

 Kila ofisa kilimo awe na shamba lake ambalo litatumika kama darasa kwa wananchi

Chapisha Maoni

0 Maoni