Unordered List


UMOJA WA VIJANA WA CCM(UVCCM) KUENDELEZA CHUO CHAKE CHA IHEMI

Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) umesema utakifufua na kukiendeleza Chuo cha Siasa, Uongozi na Ujasiriamali kilichopo Ihemi Mkoani Iringa kwa lengo la kuwapika, kuwafundisha na kuwaandaa kiujuzi na kisaikolojia vijana kwa kuwapatia  stadi za maisha ili kujitegemea kiuchumi na kujiajiri. 

Aidha Umoja huo umesisitiza kuwa Chuo hicho pia kitawaelimisha Vijana nchini kuhusu itikadi ya chama, Siasa ya chama , Ujasirimali na Uzalendo ili kujitambua na kuwa tayari kukitetea chama chao kwa nguvu ya hoja mahali popote na kujituma kwa kujiamini . 

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM  Shaka Hamdu Shaka alipozungumza na viongozi wa Matawi na Kata wa UVCCM  katika ukumbi wa Texas huko Manzese walikoshiriki semina elekezi ya ujasiriamali Mkoani Dar es Salaam. 

Shaka alisema hakuna Taifa lolote duniani lenye uwezo wa kuwapatia ajira Vijana wote badala yake huwezeshwa kielimu na kufundishwa stadi za maisha, ufanyaji bora wa biashara, uendeshaji miradi, kutambua na kuzingatia vyema miiko ya chama, siasa  na itikadi.

Alisema njia pekee ya kumuunga mkono Rais Dkt.John Pombe Magufuli na kuinua maisha ya vijana dhidi ya kadhia ya umasikini na matumizi bora ya maliasili na rasilimali za Taifa ili  Vijana wenyewe kujitambua,kujituma na kujitegemea. 

"Ili vijana waendesha miradi yao ya kiuchumi na kuwapa manufaa, biashara na kujitegemea, wanahitaji kujengwa uwezo, kupewa mbinu za kisasa na kufundishwa stadi za maisha kwa weledi na umakini "Alisema Shaka. 

Alieleza kuwa Chuo hicho sasa licha ya kutumika kuwafundisha ujasirimali vile vile kitafundisha siasa ya chama, itikadi, na uzalendo ikiwemo na kiwaelemisha katika masuala ya kujitegemea na kiufundi. 

Shaka alisema ili kuunga mkono  jitahada za Rais Dk John Magufuli ni vijana wenyewe kufanya kazi kwa bidii wanapokuwa aidha viwandani, mashambani au kushiriki  kazi za ujasirimali huku wakiwa na elimu ya kutosha,maarifa na ufahamu. 
Chuo hicho cha Ihemi kinatarajiwa kufunguliwa tarehe 5 Agosti mwaka huu.

Akizumgumzia maendeleo ya uchaguzi ndani ya chama na jumuiya zake,Kaimu huyo katibu Mkuu aliwataka watendaji wa jumuiya kusimamia na kufuata miongozo na kanuni huku wagombea wakitakiwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Alisema uchaguzi huu ni lazima utoe viongozi wenye uthubutu,uwezo wa kuitetea jumuiya, kuipigania na kuweka katika taaswira ya kuheshimika jambo litakalosaidia kuwapata viongozi  bora, makini , wenye ujasiri na uelewa . 

Pia Shaka alisema mgombea ambaye atakayekiuka miiko na maadili, kupandikizwa na kukosa sifa,  hatagombea  badala  yake atapoteza nafasi ya kuwa mgombea wa jumuiya hiyo ya vijana ya Chama Cha Mapinduzi. 

"Nasema tena hakuna mgombea atakayepitishwa na vikao vyetu ikiwa sifa zake zina kasoro, mapungufu au za kuokotezaokoteza , tutampekua kila mgombea na tukimuona hatokani na CCM  tutamtosa bila ya kuutazama uso wake "Alisisitiza. 

Aliwataka watendaji wote wa Jumuiya kufuata kanuni na taratibu,kuacha upendeleo, kutowabeba wagombea na kuvunja kanuni za uchaguzi kwani  mambo hayo na memgine hayatavumiliwa kabisa badala yake mhusika atachukuliwa hatua za kinidhamu na kuwajibishwa. 

Katika Mkutano huo Shaka uliongozana na Mwenyekiti wa UVCCM  Wilaya ya Kinondoni Said Masanga ,Katibu Katibu Idara ya Uchumi na Uwezeshaji  Dorice Obed, Katibu Msaidizi Mkuu Mawasiliano,Katibu Msaidizi Mkuu Uhusianwa Kimataifa Ebeneze Emmanuel akiwemo na Katibu wa UVCCM wilaya ya Ubungo Leah Mbeke.

ℹSource Gazeti la Uhuru.




Vijana mbalimbali waliojitokeza katika semina elekezi ya Ujasiriamali iliyofanyika Manzese wilaya ya Ubungo jijini Dar es salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni