*Ni baada ya kulisababishia Jiji la Mbeya hasara ya sh. bilioni 63
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) mkoa wa Mbeya Bw. Emanuel Kiabo kumkamata na kumuhoji
Mheshimiwa Atanas Kapunga aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya na wenzake 11
kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 63.448.
“Serikali hii haiwezi ikawaacha
watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa
halmashauri moja. Kama wako humu ndani nagiza wakamatwe na waanze
kuhojiwa na ambao wamestaafu au kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe popote
walipo ili nao waje kuhojiwa.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
leo (Jumatatu, Julai 31, 2017) alipozungumza na watumishi wa Halmashauri
za wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano
uliofanyika ukumbi wa Benjamin Mkapa.
Wengine ni waliowahi kuwa
wakurugenzi wa Jiji hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi. Elizabeth
Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya
Ukurugenzi.
Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji,
Bw. James Jorojik pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni
Bw. Mussa Mapunda, Bw. Samweli Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi. Lydia
Herbert na Bw. Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo
bila ya kuzingatia maslahi ya Jiji pamoja Emily Maganga ambaye
hakuishauri vizuri bodi hiyo.
Waziri Mkuu amesema watumishi
hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa kuwa
wameisbabishia Serikali harasa kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la
Mwanjelwa Jijini Mbeya ambalo hadi sasa halijaonyesha tija.
Amesema mradi huo wa soko la
Mwanjelwa uligubikwa na changamoto nyingi kuanzia hatua za awali ambapo
hata uchukuaji wa mkopo haukuwa umezingatia mpango mkakati wa biashara,
hivyo kusababisha Halmashauri ya Jiji kuchukua mkopo zaidi ya kiasi
kilichokusudiwa.
Waziri Mkuu amesema mbali na
kuzidisha kiasi cha mkopo pia baada ya kukamilika kwa ujenzi watuhumiwa
hao waligushi mikataba ya upangaji, jambo ambalo ni kinyume na matakwa
ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Pia waligawa vizimba kwa wafanyabiashara
bila ya kupitia mchakato wa manunuzi.
Amesema hata wahanga ambao
walikuwepo awali kabla ya kuungua kwa soko hawakupewa kipaumbele katika
mchakato wa upangishaji wa soko jipya, ambapo kwa hali ya kawaida
ilitarajiwa wangekuwa wa kwanza kufikiriwa kutokana na hasara
waliyoipata baada ya kuunguliwa mali zao.
Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya. Bw. Amos Makalla kukutana na Madiwani wa Halmashauri
ya Jiji na kuweka mikakati na namna gani wataweza kupanga bei ya vizimba
katika soko hilo ili wafanyabiashara wapange na wao kuweze kuanza
kupata fedha za kupunguza deni.
0 Maoni