Unordered List


SERIKALI YATOA BILIONI 1.9 KUBORESHA VITUO VYA AFYA

Serikali  imepeleka Sh1.92bilioni  katika Halmashauri ya mji wa Nanyamba wilayani Mtwara kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa vituo vya afya.

Hayo yameelezwa jana Jumatano Februari 28, 2018 na Waziri Mkuiu, Kassim Majaliwa ameeleza hayo wakati akizungumza na wakazi wa halmashauri hiyo, akiwa katika ziara mkoani Mtwara.

Amesema fedha hizo zilitolewa na Serikali ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, kwamba Sh1.2bilioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kata ya Njengwa, ambapo aliwasisitiza watendaji kutobadilisha matumizi.

Amebainisha kuwa ujenzi huo utahusisha chumba cha upasuaji, maabara, chumba cha kujifungulia, jengo la mama na mtoto na wodi ya wanawake na wanaume, eneo la kuchomea taka na chumba cha kuhifhadhia maiti.

“Serikali imeamua kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao,” amesema.

Aidha, Majaliwa amewataka wananchi hao kuendelea kuiunga mkono Serikali ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.

Amesema Serikali inatarajia kuipitia upya sheria ya elimu pamoja na sheria ya mtoto ili kuweka masharti ya kumlinda mtoto wa kike hususani kudhibiti mimba kwa wanafunzi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema Serikali itawachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwapa watoto wa kike dawa za uzazi wa mpango ili kuwazuia wasipate mimba.

Amesema wanafunzi wa kike katika halmashauri hiyo wamebainika kuwa wanatumia dawa za kuzuia mimba wakiwa shuleni, hivyo kuwaruhusu kushiriki katika matendo yasiyokuwa ya kimasomo.

Amebainisha kuwa Serikali itafanya msako wa kuwatafuta wote wanaotumia dawa hizo pamoja na wanaowapa na watakaobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa sababu jambo ni hatari kwa maendeleo ya wanafunzi hao.

Chapisha Maoni

0 Maoni