Unordered List


Historia ya Noti ya Tanzania

Kwa muda mrefu fedha zilizotumia katika nchi hii zilikuwa ni sarafu. Noti za karatasi zilianza kutumika mwaka 1905 wakati wa Utawala wa Mjerumani kwa upande wa Tanganyika (Tanzania Bara). Noti hizo zilitolewa katika thamani ya Rupie 5, 10, 50, 100 na Rupie 500 kama ionekanavyo hapa chini. Noti za Rupie 500 zilikuwa chache sana na sikufanikiwa kupata picha yake.

Rupie 5


Rupie 10


Rupie 50


Rupie 100


Kwa upande wa Zanzibar, mwaka huo huo wa 1905, noti za Rupee za Kizanzibari zilitolewa katika thamani za Rupee 5, 10, 20, 50, 100 na Rupee 500 pia. Kwa bahati mbaya sikuweza kupata picha zake zote, naonyesha mfano wa noti za Rupee 5 tano tu niliyofanikiwa kupata.

5 Zanzibar Rupee



Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Serikali ya Kijerumani ilitoa noti za dharura ambazo zilikuwa ni za karatasi ya kawaida kabisa. Noti hizi zilikuwa katika thamani za Rupie 1, 5, 10, 20, 50 na Rupie 200 ingawa hizi za Rupie 200 zilikuwa adimu sana na sikufanikiwa kupata picha yake.

1 Rupie


5 Rupien


10 Rupien


20 Rupien


50 Rupien


Noti hizi za dharura zilikuwa hafifu sana na wakati mwingine zilikuwa zinafyatuliwa kwa muhuri tu kama hii hapa chini ya Rupie 1.


Inaelekea kuwa Mji wa Tabora ulikuwa na umuhimu wa pili kwa Dar es Salaam wakati wa Serikali ya Kijerumani kwa vile unaonyeshwa katika Noti zote. Kama mtakumbuka, ile sarafu ya dhahabu ya Rupie 15 ilikuwa inaitwa "Tabora Pound."


Wakati wa Utawala wa Mwingereza

Baada ya Utawala wa Kijerumani kuanguka na nchi kuchukuliwa na Waingereza mwaka 1920, kwanza nchi ilitumia Noti za Rupee za Afrika ya Mashariki na Rupee za Zanzibar ingawa Rupie za Kijerumani pia ziliendelea kutumika. Kwa upande wa Zanzibar Noti ya Rupee 1 ilianzishwa mwaka 1920. Baadhi ya noti hizo ni hizi hapa:

1 Zanzibar Rupee



1 EA Rupee



5 EA Rupee



10 EA Rupee



Katikati ya mwaka 1920, Serikali ya Uingereza ilianzisha sarafu ya pamoja kwa nchi zote za Afrika ya Mashariki iliyojulikana kama Florin ya Afrika ya Mashariki. Noti za Florini zilikuwa katika thamani za Florin 1, 5, 10, 20, 50, 100 na Florin 500, ambapo noti za kuanzia Florin 10 na kuendelea juu zilikuwa pia na thamani ya Pound (1, 2, 5, 10 na 50). Kwa vile sarafu hii haikudumu zaidi ya miezi sita, ni noti chache sana zilizotolewa, mifano ya noti hizo ni kama ifuatavyo:

1 EA Florin


5 EA Florin


Mwanzoni mwa mwak 1921, Serikali ya Kiingereza ilianzisha sarafu ya pamoja Afrika Mashariki iliyojulikana kama Shilingi ya Afrika ya Mashariki na hivyo kuondokana na Florin ya Afrika Mashariki. Shilingi ya Afrika Mashariki (baadaye nitakuwa naandika kwa kifupi tu kama Shilling) ilikuwa na thamani ya Shilingi 20 kwa Pound moja na ilikuwa imeegeshwa kwenye Pound kiasi kuwa thamani ya Shiling 20 kwa Pound haikubadilika (Hii ndiyo sababu Watanzania tuliendelea kuiita shilingi 20 kama 'Pound'). Noti za Shilingi zilizotolewa wakati huo zilikuwa za thamani za Shilingi 5, 10, 20, 100, 1,000, na Shilingi 10,000. Noti za Shilingi ishirini na kuendelea juu zilikuwa pia na thamani ya Pound (1, 5, 50). Noti hizi zilikuwa zimeandikwa kwa Kiingereza, Kiarabu na Kiamhara kinachotumika Ethiopia. Katika utawala wote wa Kiingereza, kulitolewa mitindo miwili tu ya noti hizo. Mtindo wa kwanza ulidumu kuanzia mwaka 1921 hadi mwaka 1958, ma mtindo wa pili ulidumu kuanzia mwaka 1958 hadi baada ya Uhuru mwaka 1964. Sura ya mbele ya noti zote ilikuwa ikionyesha Mtawala wa Himaya ya Uingereza. Sura ya nyuma kwa upande wa noti za mtindo wa kwanza ilikuwa na simba mmoja wa kiume katika eneo la Mlima Kenya. Noti zilizotolewa mara ya kwanza wakati wa Utawala wa Mfalme George wa Tano (1910-1936) ni kama ifuatavyo:

5 EA Shilling


10 EA Shilling


20 EA Shilling


100 EA Shilling


1,000 EA Shilling

(Picha hii ilipingwa wakati pesa imeshafutwa rasmi kwa kutobolewa matundu; noti halisi haikuwa na matundu hayo)
Kwa thamani ya shilingi na uchumi wa watu wakati huo, ni noti chache sana zenye thamani ya Shiling 1,000 na Shilingi 10,000 ziliingia kwenye mzunguko, na sikufanikiwa kupata noti ya Shilingi 10,000. Kwa hiyo ilipofika mwaka 1933, serikali ikaamua kusimaisha matumizi ya noti za Shilingi 1,000 ingawa zile za Shilingi 10,000 ziliendelea. Wakati wa utawala mfupi wa Mfalme Edward wa Nane mwaka 1936, hazikutolewa noti zozote. Noti nyingine zilitolewa wakati wa utawala wa Mfame George wa Sita (1936-1952), ambapo noti ya Shilingi 1 ilianzishwa. Noti hizo zilikuwa kama ifuatavyo.

1 EA Shilling


5 EA Shilling


10 EA Shilling


20 EA Shilling


100 EA Shilling


Kutokana na uadimu wake, sikuweza kupata noti za Shilingi 10,000. Hata hivyo miaka 11 ndani ya utawala wa Mfalme George wa Sita, iliamuliwa kufuta noti hizi za Shilingi 10,000 ambazo zilikuwa hazitumiki sana.

Baada ya kifo cha Mfalme George wa Sita mwaka 1952 na binti yake Malkia Elizabeth wa Pili kuchukua usukani noti zilizotolewa zilikuwa zinafanana na zile zilizokuwapo mwanzoni isipokuwa aliondoa noti ya Shilingi 1 kwenye mzunguko.

5 EA Shilling


10 EA Shilling


20 EA Shilling


100 EA Shilling




Mwishoni mwa Utawala wa Kiingereza

Hata hivyo, mwaka 1958, noti hizo zilitengezwa upya katika mtindo tofauti na zile zilizokuwapo mwanzo. Noti mpya zilikuwa na rangi nyingi huku zikionyesha mazao mbali mbali ya uchumi yaliyokuwepo Afrika ya Mashariki. Noti ya Shilingi 5 ilionyesha pamba na karafuu; noti ya Shilingi 10 ilionyesha mkonge na chai; noti ya Shilingi 20 ilionyesha kahawa na alizeti, na mwisho noti ya Shilingi 100 ilionyesha minazi, miwese na pareto. Inaelekea kuwa kuanzia hapo, shilingi ya Afrika Mashariki iliacha kubebeshwa kwenye pound kwa vile noti mpya hazikuwa na thamani ya pound tena.

5 EA Shilling


10 EA Shilling


20 EA Shilling


100 EA Shilling


Noti hizi ziliendelea hadi baada ya Uhuru ingawa mwaka 1961 zilifanyiwa marekebsihao madogo kwenye sura ya mbele ili kuweza kuonyesha sahihi sita za Wajumbe wa Bodi ya Fedha ya Afrika Mashariki ambapo wakati huo walikuwa wameongezeka na kuwa sita kutoka watano waliokuwepo mwaka 1958. Mabadiliko hayo ni kama ifuatavyo:

5 EA Shilling


10 EA Shilling


20 EA Shilling



100 EA Shilling


Baada ya nchi zote za Afrika ya Mashariki kuwa huru, noti za kwanza zilizotolewa mwaka 1964 zilifanyiwa mabadiliko makubwa sana. Kwanza, noti hizi zilikuwa zimeandikwa katika Kiingereza, Kiarabu na Kishwahili; halafu sura ya Mtawala wa Uingereza iliondolewa na badala yake kuwekwa mashua. Sikuweza kufahamu mara moja kwa nini waliamua kutumia mashua. Sura za nyuma za noti ziliendelea kuonyesha mazao mbalimbali ya Afrika ya Mashariki ingawa kwa mpangilio tofauti kama ionekanavyo katika picha hizi.

5 EA Shilling


10 EA Shilling


20 EA Shilling


100 EA Shilling




Utawala wa Nyerere

Baada ya kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika ya Mashariki na kuundwa kwa Benki Kuu za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 1966, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa noti za kwanza zenye thamani hizo hizo za Shilingi 5, 10, 20 and Shilingi 100. Upande wa mbele wa noti hizi kulikuwa na sura ya Mwalimu Nyerere wakati wa kupata Uhuru, na upende wa nyuma ulionyesha mambo mbalimbali yaihusuyo Tanzania. Noti ya Shilingi 5 ilikuwa na Mlima Kilimanjaro, noti ya Shilingi 10 ilikuwa na shamba la mkonge, wakati noti ya Shilingi 20 ilikuwa inaonyesha mgodi wa almasi wa Mwadui. Noti ya Shilingi 100 ilikuwa inaonyesha morani wa Kimasai akichunga ng'ombe wake (Hii ilifahamika sana kama Noti ya Mmasai).

5 Tz Shilling


10 Tz Shilling



20 Tz Shilling


100 Tz Shilling


Kwa waliotumia noti hizo wanakumbuka kuwa noti ya Shilingi 10 ilikuwa inajulikana pia kama 'Jani la Katani', wakati ile ya Shilingi 100 ilikuwa inajulikana pia kama 'Masai' au 'Pink' kutokana na rangi yake. Kwa muda mrefu noti ya Shilingi 20 imeendelea kujulikana kama pound au "mbao" kutokana na historia kuwa mwanzoni ilikuwa ina thamani ya Pound 1.
Hata hivyo sura ya Masai kwenye noti ilileta mjadala kidogo kiasi kuwa Benki Kuu iliamua kuzibadilisha. Ilipofika mwaka 1969, wakatoa noti za Shilingi 100 ambazo zilikuwa na wanyama katika Mbuga ya Serengeti kama ionekanavyo hapa chini:

100 Tz Shilling


Noti hizi ziliendelea kutumika hadi mwaka 1978 zilipofanyiwa mabadiliko makubwa hasa ili kuondoa sura ya kitoto ya Nyerere na kuweka picha ya Nyerere akiwa mtu mzima. Noti mpya zote zilikuwa zimendikwa kwa Kiswahili tu, na vile vile noti ya Shilingi tano ilisimamishwa. Upande wa nyuma wa noti zote kulikuwa na Ramani ya Tanzania pamoja na sura mbalimbali zihusuzo Tanzania. Noti ya Shilingi 10 ulikuwa na Mlima Kilimanjaro, kinyago cha kimakonde na mnara wa Azimio la Arusha; noti ya Shilingi 20 ilikuwa na kiwanda cha nguo kuashiria kuwa nchi ilikuwa inasonga mbele katika viwanda, na ile noti ya Shilingi 100 ilikuwa na tasisi za elimu kuanzia shule za msingi na vyuo vikuu kuashiria juhudi za nchi kupambana na adui ujinga. Vile vile shughuli za elimu ya kujitegemea zimeonyeshwa kwa wanafunzi kulima kwa jembe la mkono!

10 Tz Shilling


20 Tz Shilling


100 Tz Shilling


Miaka saba baadaye, mwaka 1985 (muda mfupi sana kabla Nyerere hajastaafu) noti zilifanyiwa mabadiliko tena kwa kuondoa noti ya Shilingi 10 na kuwekwa kwa noti ya Shilingi 50. Noti hizi zilikuwa na sura ya Nyerere akiwa ameanza kuzeeka, na zilitumia rangi nyingi sana kuliko zilizotangulia. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958, noti ya Shilingi 100 ilibadilishwa rangi kutoka "pink" na kuwa ya bluu. Noti ya Shilingi 20 ilionyesha shughuli mbalimbali za baadhi ya viwanda vyetu, wakati Shilingi 50 ilionyesha shughuli za kujitolea kujenga mashule. Noti ya Shillingi 100 ilionyesha wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadhi ya majengo ya chuo hicho. Nadhani ilikuwa pia kuonyesha kuwa nchi imepiga hatua katika upande wa elimu ya juu.

20 Tz Shilling


50 Tz Shilling


100 Tz Shilling


Utawala wa Mwinyi

Mwishoni mwa mwaka 1985 Nyerere alirudi kijijini kwake Butiama na kuiacha Ikulu mikononi mwa Mwinyi. Noti mpya zilizotolewa mwishoni mwa mwaka 1986 zilikuwa sawa kabisa na zile zilizoachwa na Nyerere isipokuwa zilikuwa na sura ya Mwinyi isipokuwa noti zile za Shilingi 100 ambazo ziliendelea kuwa na sura ya Nyerere kama Baba wa Taifa. Vile vile noti mpya ya Shilingi 200 ilianzishwa ikiwa inajulikana wakati huo kama "double cabin." Nyuma ya noti hizi za Shillingi 200 kulikuwa na wavuvi wanaodhaniwa kuwa walikuwa wa Zanzibar kwa vile kuna karafuu inayoonekana kwa pembeni.

20 Tz Shilling


50 Tz Shilling


100 Tz Shilling


200 Tz Shilling

Ilipofika mwaka 1988, kufuatia kushuka kwa thamani ya shilingi, ilikuwa ni muhimu kuwepo kwa noti zenye thamani kubwa zaidi ili kuwapunguzia watu mzigo wa pesa. Hivyo Benki Kuu ikaanzisha noti mpya za Shilingi 500, ambao zilijulikana kama "Pajero." Noti hizi za Shilingi 500 zilikuwa na sura tofauti kabisa na zile nyingine. Nembo ya Taifa ilikuwa ya rangi, halafu zilikuwa na nembo ya waziwazi ya Benki Kuu ya Tanzania. Nyuma yake zilionyesha akina mama wakivuna zao la kahawa au karafuu, sikumbuki tafsri ya picha hiyo vizuri.

500 Tz Shilling


Kasi ya kupungua kwa thamani ya shilingi ilikuwa kali sana kiasi kuwa miaka miwili baadaye, yaani mwaka 1990, Benki Kuu ililazimika kuingiza noti mpya ya Shilingi 1,000 ambayo ilikuwa na sura kama ile ya Shilingi 500 isipokuwa ngao ya taifa haikuwa ya rangi. Vile vile ilikuwa na maandishi ya ndani kwa ndani (water mark) kuonyesha 1,000. Nyuma yake kulikuwa kiwanda cha nyama cha Tanganyika Packers cha pale Kawe.

1000 Tz Shilling


Noti zetu wakati huo zilikuwa pana sana na zilikuwa zinaongezeka upana kadiri thamani yake inavyopanda. Ilipofika mwaka 1992, Benki Kuu ilifanya mabadiliko makubwa katika noti zetu. Kwanza zilipunguzwa sana upana halafu zote zikatengenezwa upya kuwa na sura inayofanana. Noti ya Shilingi 20 iliondolewa na badala yake zikaongezwa noti mbili za Shilingi 5,000 na Shilingi 10,000 kama ifuatavyo:

50 Tz Shilling


100 Tz Shilling


200 Tz Shilling


500 Tz Shilling


1000 Tz Shilling


5000 Tz Shilling


10000 Tz Shilling



Noti hizi ziliendelea kutumiwa hadi mwisho wa utawala wa Mwinyi mwaka 1995.


Utawala wa Mkapa na Kuendelea Hadi Leo

Wakati Mkapa alipochukua usukani wa kuongoza nchi mwaka 1995, aliamua kusitisha matumizi ya sura za viongozi kwenye noti (kwa kuwa yeye hakutaka iwekwe sura yake, kama alivyokataa kuitwa 'mtukufu rais' bali 'mheshimiwa rais'). Kwa hiyo noti zote zilizotolewa mwaka 1997 chini ya utawala wake hazikuwa na sura ya kiongozi yeyote. Badala yake zilikuwa na kichwa cha Twiga ambaye kihistoria ndiye Mnyama wa Taifa. Wakati huo pia, noti za Shilingi 50, 100 na Shilingi 200 zilisimamishwa.

500 Tz Shilling


1000 Tz Shilling


5000 Tz Shilling


10000 Tz Shilling


Hata hivyo, baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka 1999, iliamuliwa kuwa sura yake iwe ya kudumu kwenye noti ya Shilingi 1,000, hivyo noti hiyo ilisanifiwa upya na kuwa kama ifuatavyo:

1000 Tz Shilling


Noti hizi ziliendelea kutumika hadi mwaka 2003 zilipofanyiwa mabadiliko ya kuongeza usalama zaidi. Vile vile kutokana na manung'uniko ya kichinichini kutokea Zanzibar kuhusiana na mtumizi ya Twiga ambaye alikuwa mnyama wa Tanganyika, iliamuliwa kutotumia twiga tena. Badala yake sura za wanyama wakubwa mbalimbali wa Tanzania zilitumika ingawa sura ya Nyerere iliendelea kubaki kwenye noti za Shilingi 1,000. Vile vile noti mpya ya Shilingi 2,000 ilianzishwa. Upande wa nyuma wa noti hizi ulionyesha shughuli mbalimbali za uchumi, sehemu za kihistoria na harakati za kukuza elimu. Kwa mara nyingine tena kuanzia mwaka 1978, noti hizi ziliandikwa kwa Kiingereza na Kishwahili tena. Noti hizi ndizo zinazotumika hadi leo, sura zake ni kama ifuatavyo:

500 Tz Shilling


1000 Tz Shilling


2000 Tz Shilling


5000 Tz Shilling


10000 Tz Shilling


Hatujui mabadiliko yajayo yatakuwaje hasa ikizingatiwa kwamba Shilingi yetu imeendelea kuporomoka thamani kila mwaka. Tusubiri na tuone.

Chapisha Maoni

0 Maoni