Unordered List


WAZIRI DKT. MAGUFULI AZINDUA UJENZI WA BARABARA ZA PETE JIJINI DAR ES SALAAM.


Waziri wa Ujenzi Mheshimkiwa Dkt.John Pombe Magufuli leo amezindua na kuweka  mawe ya msingi katika Ujenzi wa barabara za pete zitakazopunguza msongamano jijini Dar es salaam.
Barabara hizo zilizowekewa mawe ya msingi ni pamoja na ile ya  Kinyerezi –Kifuru hadi Mbezi Mwisho yenye urefu wa kilometa 14.0, Kigogo-Tabata Dampo yenye urefu wa kilometa 1.6, na Kimara Baruti-Msewe hadi Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 2.6. Barabara nyingine ni ile ya External –Kilungure hadi Kimara Korogwe kilometa 8.0, Wazo Hill-Goba hadi Mbezi mwisho kilometa 20 na Goba-Tangi bovu kilometa 9.0.
Akizungumza wakati akizindua ujenzi wa barabara hizo Waziri Magufuli amewataka wananchi kufuata sheria za barabarani kwa kutoingilia hifadhi za barabara na wale wenye nyumba pembeni mwa barabara kuzibomoa wenyewe ili kupisha ujenzi huo kwenda kwa wakati.

“Nawahakikishieni kwamba mkifuata sheria za kutojenga karibu na barabara barabara hizi zitajengwa kwa kiwango cha lami na kwa wakati ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu na ninyi mtanufaika na fursa za kibiashara kwa kuwa karibu na barabara za lami na hivyo kujikwamua kiuchumi”,amesisitiza Waziri Dkt. Magufuli.

Waziri Magufuli amesema barabara ya Wazo HilL –Goba yenye urefu wa kilometa 20 ikikamilika kwa kiwango cha lami itaziunganisha barabara za Bagamoyo na Morogoro ambazo zimekuwa zikikabiliwa na msongamano kwa muda mrefu.

Aidha, amesema barabara ya Kinyerezi- Kifuru hadi Mbezi mwisho yenye urefu wa kilometa 14 itapunguza pia msongamano kwa kiasi kikubwa kwa kuwa itakuwa inaunganisha barabara ya Morogoro na Nyerere hivyo kuwataka wananchi kuanza kuzitumia barabara hizo ambazo zitakamilika kwa wakati.

Chapisha Maoni

0 Maoni