Atakumbukwa kwa mema aliyoitendea jumuiya.
Na Mwandishi wetu Iringa
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umepokea kwa
huzuni , masikitiko na fazaa taarifa ya kifo cha aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Farouz aliyefariki usiku wa
kuamkia leo na kuzikwa (adhuhuri) mchana huu katika makaburi ya
Mwanakwerekwe kisiwani Unguja.
Tanzia ya UVCCM iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM
Shaka Hamdu Shaka kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM
)Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana Ofisi ndogo ya CCM Lumumba imeeleza
kuwa kifo hicho ni pigo kwa CCM na jumuiya zake.
Shaka alimueleza Kinana kwamba marehemu Ferouz ni zao la
juhudi na maandalizi ya Chama cha Mapinduzi kwa vijana wake na kwamba
utumishi wake toka akiwa UVCCM hadi kufikia Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar kwa miaka kumi mfululizo ni kielelezo cha kutosha katika
utendaji wake uliotukuka.
Amesema vyovyote itakavyokuwa kifo cha mwanasiasa huyo
licha ya kuacha pengo ambalo litakawia kuzibika, atakumbukwa kwa tabia
yake ya kupenda Umoja, muungano, kujichanganya na kutopindisha maneno
katika jambo lenye maslahi kwa Taifa.
"UVCCM tumepokea kwa huzuni na fazaa kubwa taarifa za kifo
cha kada wa chama chetu, kiongozi jasiri na mwanasiasa mpiganaji shupavu
kwa maslahi ya Taifa na mweledi katika uchambuzi wa masuala ya kisiasa
"alisema shaka
UVCCM imeisihi familia yake, wana CCM na watanzania wapenzi
wa Umoja , amani na mshikamano kuwa na subira, uvumilivu na utulivu
katika wakati huu mgumu wa msiba na maombolezo .
"Yapo mambo mengi ya kujifunza unapoyatazama na kuiakisi
safari ya kisiasa ya Saleh Ramadhani Ferouz katika maisha yake hadi kifo
kumkuta, hatutaacha wala kubeza lolote jema alilolifanya katika
kipindi cha uongozi wake na ushiriki wake katika maisha ya
siasa"alisisitiza .
Shaka alisema UVCCM inaungana na familia ya marehemu katika
kipindi hiki lilichogubikwa na kiwingu cha huzuni kufuatia kifo cha
mwanasiasa huyo ambaye amewahi kutumikia UVCCM katika nyadhifa mbali
mbali ikiwemo mwaka 1989 aliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi Idara ya
Fedha na uendeahaji Makao Makuu UVCCM, mwaka 1993 akawa Katibu msaidizi
Mwanadamizi Idara ya Oganaizesheni na Utawala akishughulikia Utumishi
UVCCM Makao Makuu.
Kutoka na juhudi ari na moyo wa kujituma Marehemu Feruzi
Mwaka huo huo akapandishwa daraja na kuwa Mkuu wa kitengo cha Utumishi
UVCCM Makao Makuu ambapo mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi
UVCCM Afisi Kuu Zanzibar na Mwaka 1999 aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu
wa UVCCM Zanzibar na baadae aliteuliwa Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar
kazi ambayo alifanya kwa mafanikio makubwa akidhihirishia ulimwengu kuwa
amepita na kuokwa katika tanuri la kuandaa viongozi (UVCCM) kama
ilivyokuwa kwa viongozi wengine katika chama na Serikali.
Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu Saleh Ramadhan Ferouz peponi.
Inna Lilahi wa Inna Ileihiy Rajiun
0 Maoni