Serikali
imewapandisha madaraja watumishi wa umma 113,520 walioajiriwa mwaka
2012 katika awamu tatu, ambapo ya kwanza walipandishwa vyeo Watumishi
28,049 waliokuwa wameidhinishiwa vyeo kabla ya zoezi la uhakiki wa
watumishi hewa na uhakiki wa vyeti kuanzia mwezi Juni, 2016, awamu ya
pili ilianza mwezi Novemba, 2017 na ilihusisha watumishi 59,967 ambao
taarifa zao zilikuwa kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na
Mishahara (HCMIS) kabla ya zuio na awamu ya tatu ilianza mwezi Aprili,
2018 na ilihusisha Watumishi 25,504 ambao barua zao zilikuwa
hazijaingizwa kwenye Mfumo.
Ufafanuzi
huo, umetolewa Bungeni jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary M. Mwanjelwa (Mb) wakati
akijibu swali la Mhe. Joram Hongoli (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
lililohusu watumishi wa umma walioajiriwa 2012 kutopandishwa madaraja
mpaka hivi sasa.
Dkt. Mwanjelwa alisema, watumishi walioajiriwa Mwaka 2012 walistahili kupandishwa madaraja kuanzia mwaka 2016/2017 kipindi ambacho Serikali ilikuwa ikifanya zoezi la uhakiki wa watumishi hewa na uhakiki wa vyeti, hivyo mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Serikali ilianza kuwapandisha watumishi hao kwa awamu hizo tatu kwa kuzingatia vigezo stahiki na kuongeza kuwa watumishi wengine ambao wamekidhi vigezo wataendelea kukasimiwa katika bajeti ya mishahara ili waweze kupandishwa vyeo katika mwaka huu wa fedha 2018/2019.
Aidha,
Dkt. Mwanjelwa aliainisha kuwa, watumishi 31,188 walioajiriwa na
TAMISEMI mwaka 2012, kati ya hao watumishi 15,320 wamepandishwa vyeo na
kubadilishiwa mishahara, na watumishi 3,349 waajiri wao wamewapandisha
vyeo lakini majina yao yapo UTUMISHI kwa ajili ya kupitia taarifa zao
kabla ya kuwabadilishia mishahara na watumishi 1,064 waliopandishwa
vyeo wamebainika kuwa na hoja mbalimbali ambazo waajiri wanapaswa
kuzikamilisha na kurejesha majina yao UTUMISHI kwa ajili ya
kuwaidhinishia mishahara.Watumishi 4,552 hawapo tena katika Utumishi wa
Umma na watumishi 6,903 bado hawajapandishwa vyeo ambapo Serikali
inatarajia kuwapandishwa vyeo wakati wowote katika mwaka huu wa fedha
2018/19.
Suala
la upandishwaji vyeo kwa Watumishi wa Umma linazingatia vigezo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na utendaji kazi mzuri, kukidhi sifa
zilizoainishwa katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, uwepo wa nafasi
wazi na bajeti iliyotegwa.
Kwa
mujibu wa Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, mtumishi anapaswa kutumikia
cheo kimoja si chini ya miaka mitatu kabla hajafikiriwa kupandishwa
cheo.
Aidha,
iwapo mtumishi ameajiriwa kwa mara ya kwanza atapaswa kumaliza mwaka
mmoja wa kuthibitishwa kazini kisha ndipo atumikie cheo hicho si chini
ya miaka mitatu, hivyo kwa kuzingatia sifa mtumishi anaweza kupandishwa
cheo baada ya miaka 3, 4, 5 au hata saba kutegemea na kukidhi vigezo
stahiki.
Imetolewa Na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi Ya Rais (Utumishi)
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi Ya Rais (Utumishi)


0 Maoni