Unordered List


Serikali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya ugonjwa wa Dengue


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya ugonjwa wa Dengue kwa kununua vipimo 30,000 vya ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Mohhamad Bakari Kambi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mapema jana katika ofizi ndogo za Wizara Jijini Dar Es Salaam.

Prof. Kambi amesema kuwa vipimo hivyo tayari vimeshanunuliwa na vitaingia nchini hivi karibuni na kusambazwa kwenye vituo vya umma Jijini Dar Es Salaam pamoja na mikoa mingine yenye athari za ugonjwa huo.

Amesema kuwa ugonjwa wa dengue hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja na kuwataka wananchi kuacha kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu tiba za ugonjwa huo.

Mganga Mkuu amesema kuwa mpaka sasa vituo vinavyopima ugonjwa wa homa ya Dengue katika Mkoa wa Dar es Salaam ni Muhimbili, Maabara kuu Muhimbili, Amana, Temeke, Mwananyamala, Sinza, Vijibweni, Mnazi mmoja, Lugalo, Mbagala, FFU Ukonga. Katika mkoa wa Tanga; vituo vya Bombo na Horohoro, vituo vingine ni Tumbi Mkuranga, Utete Rufiji na Mafia, Morogoro na Manyara Aidha natambua vipo pia vituo binafsi vinavyotoa huduma za upimaji. Katika mikoa mingine ufuatiliaji unaendelea na hatujapa wagonjwa wenye dalili za Homa ya Dengue.

Aidha Prof. Kambi amesema kuwa Wizara inatambua juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Dar Es Salaam na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayofanya ya udhibitiwa ugonjwa huo kupitia zoezi la kunyunyizia dawa viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu sambamba na elimu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Yudas Ndungile amesema kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaojitokeza katika vituo vya afya kupata vipimo ni kutokana na wananchi kupata uelewa wa ugonjwa huo baada ya kupatiwa elimu dhidi ya ugonjwa huo. “Tumepita kwenye maeneo ya kata zenu kufanya uelimishaji wa namna ya kujikinga na kutambua dalili za ugonjwa huu” amesema Dkt. Ndungile na kuendelea kusema kuwa vyombo vya habari vimetoa mchango mkubwa kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa dengue.

Chapisha Maoni

0 Maoni